Facebook

Sunday, 13 April 2014

LIVERPOOL YAZIDI KUJIIMARISHA KILELENI

Liverpool imezidi kujiimarisha kileleni mwa ligi kuu ya England baada ya kuicharaza Manchester City magoli 3-2 katika mchezo mkali uliochezwa uwanja wa Liverpool, Anfield Jumapili.
Liverpool ilianza kuhesabu magoli yake katika dakika ya sita likifungwa na Sterling. Skrtel alizidi kuisononesha Manchester City baada ya kupachika goli la pili kwa njia ya kichwa kufuatia mpira wa kona langoni mwa Manchester City.
Hadi mapumziko Liverpool 2, Manchester City 0.
Manchester City walizidi kupata pigo baada ya kiungo wao maarufu Yaya Toure kuumia na kulazimika kutoka nje.
Kipindi cha pili Manchester City waliimarika zaidi na kulishambulia lango la Liverpool na kuweza kupata goli la kwanza likifungwa na David Silva dakika ya 57. City walizidisha mashambulio katika lango la Liverpool na katika harakati za kuokoa kombora la Silva, Johnson alijifunga na kufanya matokeo yawe 2-2 hadi kufikia dakika ya 62.
Manchester City walizidi kulisakama goli la Liverpool na kukosa magoli.
Kosa la nahodha wa Manchester City Vincent Kompany katika kuondoa mpira kulisababisha timu yake iadhibiwe na kombora la Philippe Coutinho, kabla ya Liverpool kumpoteza mchezaji wake Jordan Henderson aliyepigwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea vibaya mchezaji wa Manchester City.
Kwa matokeo hayo Liverpool inaongoza ligi kuu ya England kwa pointi 77 baada ya michezo 34 ikifuatiwa na Chelsea yenye pointi 72 ambayo nayo inacheza Jumapili mchezo wake wa 34, nafasi ya tatu ikishikiliwa na Manchester City yenye pointi 70 baada ya mechi 33, huku Everton ikikalia nafasi ya nne na pointi 66, Arsenal ikiwa imeshuka hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi 64.

0 comments:

Post a Comment