Shirika la Utangazaji Nchini (TBC) jana
limevuruga mwenendo wa Bunge la Katiba baada ya kukata matangazo yake
wakati mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu Lissu alipotoa ufafanuzi wa
maoni ya walio wachache.
Mgogoro huo ulitokea bungeni jana wakati Tundu
Lissu akitoa ufafanuzi kuhusu maoni ya wajumbe walio wachache wa kamati
namba nne.
Wakati Lissu akiendelea na ufafanuzi huo, baadhi ya wajumbe walianza kunong’ona kuwa TBC imesitisha matangazo.
Hata hivyo, kauli hiyo ilimfanya Lissu kudharau na kuendelea na ufafanuzi wake.
Baada ya muda mfupi alisimama mjumbe wa Bunge
hilo, Freeman Mbowe na kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo
kuhusiana na tukio hilo.
“Mjadala huu ni muhimu sana na mjadala huu umekuwa
ukirushwa na kituo cha televisheni cha Taifa TBC muda wote tangu
tumeanza. Hivi punde kuna taarifa kuwa TBC wamekata matangazo yote ya
Redio na Televisheni una nini cha kuwaeleza Watanzania?”alihoji Mbowe.
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo,
Samuel Sitta, alisema taarifa ya TBC kufunga matangazo ni ya kushtua
sana kwa sababu Bunge Maalumu lina mkataba na serikali pamoja na TBC One
wa kuhakikisha mjadala na matangazo yote ya Bunge hilo yanaonekana na
kuwafikia wananchi.
“Naomba Katibu achunguze mara moja, aangalie nini
kimetokea kama ni tatizo la muda ama la kiufundi na tutapata majibu sasa
hivi,”alisema na kulazimu Bunge hilo kusimama kwa muda.
Baada muda mfupi, Sitta alisema tatizo ni hali ya hewa jijini Dar es Salaam.
“Katibu amepanda huko juu katika studio na maelezo
ya kitaalamu yanasema hali ya hewa Dar es Salaam,” alisema kauli
iliyoamsha kelele kutoka kwa baadhi ya wajumbe hao huku wengine
wakisikika wakisema barabara zimekatika na uwanja wa ndege umefungwa
jana.
Hali hiyo ilimbidi Sitta kuwasihi wajumbe hao kutulia kwa sababu mambo yote yangetengezwa.
“Ni hivi kwa sababu yoyote ile hatuwezi
kuendelea,” Hali hiyo iliibua nderemo na vifijo kutoka kwa baadhi ya
wajumbe huku wakitamka “Sitta, Sitta, Sitta.”
0 comments:
Post a Comment