VIONGOZI wanne wa kitaifa, wamenusurika kufa baada ya helikopta
waliyopanda kwa ajili ya kukagua na kuangalia athari za mafuriko jijini
Dar es Salaam, kuanguka wakati ikitaka kuruka.
Helikopta hiyo ambayo inaelezwa kwamba ndiyo kwanza ilikuwa inaanza
kuruka, ilianguka ghafla baada ya kutokea hitilafu katika injini yake.
Viongozi walionusurika kifo katika ajali hiyo ya helikopta mali ya
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni Makamu wa Rais Dk. Mohamed
Gharib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Ndani ya helikopta hiyo, alikuwemo pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadik, waandishi wa habari wawili na maofisa wengine kutoka
ofisi ya Makamu wa Rais ambao idadi yao ilikuwa 11.
Wengine walionusurika ni marubani (wawili), walinzi wa viongozi (wawili) na ofisa mmoja kutoka Ikulu.
Waandishi wa habari waliokuwa katika helikopta hiyo ni mpiga picha wa
kituo cha Channel Ten, Khamis Suleiman na George Kasembe wa TBC.
Taarifa zinaeleza kuwa helikopta hiyo ilipata hitilafu wakati
ilipotaka kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Jeshi (Airwing) Ukonga, Dar
es Salaam na kushindwa kuruka.
Mtoa taarifa wa tukio hilo ambaye hakutaka kutaja jina kwa kuwa si
msemaji wa jeshi hilo, alisema hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa
viongozi hao na wengine, lakini walipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya zao.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Kamanda wa Polisi wa
viwanja vya ndege nchini, Khamis Suleiman, alisema ajali hiyo
iliyohusisha helikopta namba JWTZ 9505, ilitokea jana, majira ya saa
3:25 asubuhi.
“Ni kweli ajali imetokea na baadhi ya waandishi waliokuwemo kwenye
helikopta hiyo ambayo uchunguzi wa awali unaonyesha ilipata hitilafu
wakati inaruka,” alisema Kamanda Suleiman.
Aliongeza kuwa viongozi hao waandamizi wa serikali walikuwa katika
ziara ya kukagua maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam yaliyokumbwa
na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, ambazo hadi sasa
zimesababisha vifo vya watu zaidi ya kumi na uharibifu wa miundombinu.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, Kamanda Kova na Mwandishi wa
Channel Ten, Suleiman, walipozungumza na Tanzania Daima kwa nyakati
tofauti kuhusu hali zao, walisema wanaendelea vizuri.
Katika kuonyesha kuwa hakukuwa na madhara ya ajali hiyo, Makamu wa
Rais Dk. Bilal baada ya ajali hiyo, alikwenda kukagua maeneo
yaliyoathirika na mafuriko kwa kutumia gari baada ya helikopta hiyo
kupata hitilafu.
Taarifa ya JWTZ
JWTZ limesema kuwa helikopta hiyo ilipata ajali jana, majira ya saa 3:30 asubuhi wakati ilipokuwa katika hatua ya kuanza kuruka.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na
Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi, Upanga, ilieleza kuwa helikopta hiyo
mbali na kubeba viongozi hao, walikuwapo pia Dk. Mnzava, Msaidizi wa
Makamu wa Rais, Msaidizi wa Kamanda Kova na waandishi wa habari watatu.
“Ujumbe wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulikuwa
katika safari ya kuzungukia maeneo yaliyoathirika na mafuriko katika
Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani kutokana na mvua kubwa iliyoanza
kunyesha juzi hadi sasa.
“Makamu wa Rais pamoja na ujumbe wake hawakupata majeraha katika
ajali hiyo. Aidha, rubani na wasaidizi wake pia wametoka salama,”
ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza uchunguzi wa ajali hiyo umeanza ili kubaini chanzo chake
0 comments:
Post a Comment