MAELFU ya abiria waliokuwa wakisafiri kutoka jijini Dar es Salaam na
wengine wakitokea mikoani wamekwama kutokana na daraja la Mto Ruvu
lililopo wilayani Kibaha, Pwani kujaa maji kutokana na mvua
zinazoendelea kunyesha.
Mvua hiyo ambayo ilianza kunyesha mfululizo tangu juzi, imesababisha
uharibifu mkubwa wa miundombinu ambayo imesababisha magari makubwa na
madogo kushindwa kuendelea na safari zao.
Kutokana na daraja hilo kujaa maji, magari yaliyokuwa yakitokea Dar
es Salaam kuelekea mikoa mingine ya jirani na nje ya nchi yamekwama
katika eneo la bonde la Mto Ruvu na kusababisha foleni kubwa.
Mbali na magari hayo yaliyokuwa yakitokea Dar es Salaam kushindwa
kuendelea na safari, pia magari ambayo yalikuwa yakitokea mikoa mingine
kuelekea Dar es Salaam nayo yalikwama.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Halima Kihemba, alisema kutokana na maji
kujaa katika daraja hilo, ilibidi watoe tahadhari kwa magari yote
yanayopita katika barabara hiyo kutoendelea na safari hadi
yatakapopungua.
Alisema serikali itahakikisha inaweka utaratibu mzuri ambao utasaidia
kwa kiasi kikubwa wale wote ambao wamekumbwa na mafuriko katika nyumba
zao kutokana na mvua hizo.
Kihemba alisema kwamba kutokana na hali hiyo, wananchi wa maeneo ya
Mlandizi na mengine kuwa makini katika kipindi hiki, kwani mafuriko
yanaweza kusababisha kupoteza maisha ya watu na kuharibu miundombinu.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mlandizi, Abdallah Kido,
alisema katika mji wa Mlandizi hali ni mbaya kutokana na mafuriko hayo
kusababisha madhara makubwa kwa wananchi na magari kushindwa kuendelea
na safari.
0 comments:
Post a Comment