Watu kumi wamekufa, na mamia kukosa mahali pa kuishi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Kamishna Suleiman Kova, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo,
ambapo alisema kati ya watu hao kumi, watano ni watu wazima na watoto
watano.Daraja la Mpiji linalounganisha wilaya ya Kinondoni katika mkoa wa Dar es Salaam na Bagamoyo mkoa wa Pwani limekatika na kupoteza mawasiliano kati ya mikoa hiyo miwili.
Watu walioathirika zaidi kutokana na mafuriko hayo ni watu waliojenga mabondeni, hasa maeneo ya Jangwani, na bonde lote la mto Msimbazi.
Wakazi hawa ambao mara kwa mara hukumbwa na kadhia hii hata pale mvua ndogo zinaponyesha, hali ya sasa imekuwa tishio zaidi kwa maisha yao na mali, huku mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq akisema serikali haitaweza kuendelea kuwasaidia waathirika hawa, ambao wanapuuza wito unaotolewa mara kwa mara kuwataka kuyahama maeneo hayo hatarishi, na wengine hata kwenda mahakamani kupinga amri ya kuwataka kuhama.
Hata hivyo baadhi yao waligoma kuhama na wale waliohama wanadaiwa wengine walivitelekeza viwanja walivyogawiwa na kurejea katika maeneo yao ya mabondeni.
Mradi mwingine muhimu wa Mabasi yaendayo kasi, DART unaolenga kutatua tatizo la usafiri jijini Dar es Salaam, nao umeathiriwa na mvua zinazonyesha na kusababisha hasara ya kiasi cha dola elfu thelathini za Kimarekani kutokana na magari yake matatu kuharibiwa pamoja na mashine nyingine na mifuko ya saruji kuchukuliwa na maji hivyo kusitisha shughuli zake za ujenzi zilizo katika hatua za mwisho kukamilika kwa barabara ya Mbezi hadi Kivukoni katikati ya jiji.
Mpaka sasa mkoa wa Dar es Salaam umeripotiwa kukosa mawasiliano na mikoa mingine kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya barabara na reli.
Wakati huo huo makamu wa Rais, Dokta Mohammed Gharib Bilal, akiwa pamoja na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Sadiq Meck Sadiq na kamanda wa polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wamenusurika katika ajali ya helikopta wakati wakikagua athari za mafuriko katika mkoa wa Dar es Salaam.
Habari zinasema walipata majeraha kidogo na kuendelea na shughuli za kukagua maeneo ya mafuriko katika mkoa wa Pwani.
0 comments:
Post a Comment