AZAM FC iliweka historia mpya baada ya kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2013/14 kufuatia ushindi wa magoli 2-1
dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jana licha ya Yanga iliyo
katika nafasi ya pili nayo kushinda 2-1 dhidi ya JKT Oljoro kwenye
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Ilikuwa ni mara ya kwanza katika miaka 14 kwa timu nje ya Simba na Yanga
kutwaa taji hilo tangu Mtibwa Sugar ya Morogoro ilipolibeba mara mbili
mfululizo mwaka 1999 na 2000.
'Wanalambalamba' ambao wametwaa kombe hilo bila ya kupoteza mchezo,
waliingia uwanjani jana wakihitaji pointi tatu ili kufikisha pointi 59
ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine, walipata ushindi waliouhitaji
kwenye uwanja huo mgumu ambao wageni wa ligi Mbeya City walikuwa
hawajapoteza mchezo.
Yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa kocha Mcameroon Joseph Omog, ambaye
ameutwaa ubingwa huo katika jaribio lake la kwanza baada ya watangulizi
wake kushindwa na kuishia kushika nafasi ya pili katika misimu miwili
mfululizo iliyopita.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Azam wataiwakilisha nchi katika michuano ijayo
ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya kwanza kwao, huku Yanga
ambayo imejihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili kwa kufikisha
pointi 55, itacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Mbeya City licha ya kushiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza
imejihakikishia kumaliza katika nafasi ya tatu licha ya kipigo cha jana
ikiwa na pointi 46, ambazo haziwezi kufikiwa na timu za chini yao.
Simba iliyokuwa na msimu mbaya ambao hawatapenda kuukumbuka, ilikumbana
kipigo kingine kisichotarajiwa cha 1-0 dhidi ya Ashanti United kwenye
Uwanja wa Taifa jana na kujiweka katika hatari ya kuikosa hata ya
kumaliza katika nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo iliyobakisha mechi
moja kumalizika. Goli hilo lilifungwa na Mohammed Nampaka katika dakika
ya 17.
Gaudence Mwaikimba aliipatia Azam goli la kuongoza katika dakika ya 44
kufuatia pasi ya Erasto Nyoni lakini Mwegane Yeya ambaye aliifunga Azam
'hat-trick' katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyomalizika kwa
sare ya 3-3 kwenye Uwanja wa Azam Complex, aliisawazishia Mbeya City
katika dakika ya 70 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Aishi Manula
kufuatia shuti la Deus Kaseke. Yeya awali katika dakika ya 19 alipiga
shuti lililogonga mwamba na kuokolewa na beki wa Azam, Said Morad.
John Bocco alifunga goli lililowapa ubingwa Azam katika dakika ya 86 kwa
kichwa na kufanya mpira usimame kwa muda wachezaji wa Mbeya City
wakipinga bao hilo.
Mjini Arusha, Yanga walitangulia kufungwa kwa goli katika dakika ya 68
lakini walisawazisha dakika mbili baadaye kupitia kwa mtokeabenchini
Rajab Zahir akiunganisha kwa kichwa mpira wa 'fri-kiki' uliopigwa na
Juma Abdul na Mrisho Ngasa akafunga la ushindi katika dakika ya 73
akiunganisha kwa mguu mpira wa kona ya Simon Msuva.
Mgambo na Kagera Sugar zilitoka 0-0, wakati Ruvu Shooting ilishinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwa goli la Elias Maguli (dk.36).
Matokeo yalimaanisha kwamba Oljoro na Rhino zimeshuka daraja.
0 comments:
Post a Comment