Facebook

Tuesday, 15 April 2014

RAGE AMESOMA NA KUELEWA KITABU CHA KROENKE NA HILLWOOD


Miaka 12 iliyopita nilikua na umri wa takribani miaka 8,Katika umri huo nilikua na akili ya utambuzi wa mema na mabaya.Darasa langu la tatu lilitosha kujua nini Wazazi wanapenda nifanye na nini hawataki kusikia nafanya. Japo ilikua ngumu kutimiza matakwa yote ya wazazi ila nilijaribu kuwaridhisha.Kati ya mambo ambayo wazazi wangu walichukia ni mchezo wa mpira wa miguu,hapo ndo kulikua na kazi,nilipopenda sana wao ndipo walipochukia sana.

                      Nikakubali kuitwa mtoto msumbufu,mjeuri,mkaidi na majina mengine mengi mabaya kwa ajili ya huu mchezo. Wazazi hawakuishia hapo kila waliposikia nimeenda kucheza mpira jioni yake sebule hujaa fimbo nyingi,ungefikiri sungusungu wanafanya maandalizi kwa ajili ya kwenda kukamata na kupiga waarifu usiku huo,La hasha fimbo zote zilikua zinasubiri mwili wangu mdogo mfano wa fidodido. Nakumbuka nilikua Napata kipigo mithili ya mbwa mwizi. Lakini fimbo hizo hazikunizuia kesho yake kuibuka kwenye kiwanja changu cha koloni kilichopo mpakani mwa Vingunguti na Tabata na kuendelea kula ladha za sembo,nyuzi banana au kipere pasi na kukumbuka kipigo cha jana nillichopewa na Bi mkubwa.
                     Kabumbu litasakatwa mpaka mishale ya saa 12 na nusu jioni. Kila mmoja na njia yake kuelekea nyumbani kwake,hapo ndipo mafua ya ghafla yanaponianza sambamba na moyo kudunda mara 180 kwa dakika,huku nikihisi kibofu cha mkojo kinataka kupasuka. Hiyo ilikua ni hofu ya bakora kutoka kwa mama au baba. Nisipowakuta wazee nyumbani hua nafanya kazi nyingi za nyumbani hata zile zisizonihusu ili nifunike kombe mwanaharamu apite. Lakini sikuweza kuwashawishi mahakimu wangu kuwa huru na adhabu ya bakora.Ikafika kipindi ikawa ratiba niliyoizoea,Asubuhi naenda shule nikitoka shule naelekea viwanja vya soka nikirudi nyumbani nachezea fimbo kabla ya kwenda kulala.
                    Nikaendelea kukua kiumri pia kiakili,Siku moja nikamuweka mama kitako na kumuuliza “Mama kwanini hutaki na upendi nicheze mpira?” Mama akanijibu “nakupenda sana mwanangu,sitaki uharibikiwe kama watoto wengine (huku akitoa mifano ya watoto hao kwa majina),wamepoteza muda wao mwingi kwenye michezo,shule imewashinda ona walivyo sasa hawana mbele wala nyuma(mama aliendelea)” Akaniuliza na wewe unataka kuja kua kama wao? Nikajibu kwa haraka “hapana mama”  “basi mwanangu soma sana ili uje kuwa daktari,engineer,au mwalimu achana na habari za mpira hakuna mtu aliyefanikiwa kwa mpira  wa miguu”.Maneno ya mama yaliniingia na kugusa moyo wangu,hasa pale nilipogeuza shingo yangu na kuanglia maisha ya wachezaji soka mashuhuri mtaani kwangu,niliangalia maisha ya Athumani Machepe aliyekua akiichezea Simba, sikuona tofauti yake na kijana asiye na ajira kwa kipindi hicho. Si Machepe peke yake bali kuna wachezaji wengi wa miaka ya nyuma walipata kuwa maarufu sana huku mifuko yao ya suruali ikiwa imetoboka.Hao ndo wasakata kabumbu wa zamani,walikua na uzalendo na mapenzi thabiti na soka.
             Achana na Habari za mwanzoni mwa karne ya 21,Siku hizi kuna MAONO MAPYA YA DUNIA. Ndani ya maono  hayo kuna bosi na kiongozi mmoja tu. Bosi huyo ana majina mengi kwa kila nchi na kwa kila kabila,wengine watamuita maela,faranga,kwacha,yen,dollar,shilingi na kwa majina ya jumla anaitwa money au Pesa. Majina ya bosi huyu ni mengi lakini yana maana,Lengo na kazi zinazofanana.Miaka ya nyuma ili uheshimike kwenye jamii ilikua lazima uwe na Elimu,Hapo utashinda dhidi ya umma. Lakini Maono mapya ya Dunia Hayatambui Elimu juu  ya heshima, Maono mapya ya Dunia yanaamini Mtu mwenye busara,Hekima na kustahili  Kuheshimiwa ni Yule mwenye pesa. Uingineer,Udaktari,ualimu wako bila shekeli hakuna atakayetambua,kuthamini wala kuheshimu taaluma yako.

                    Kwenye Dunia yetu mpya kila kitu pesa.Kinachonifurahisha zaidi hata kwenye ulimwengu wetu wa soka pesa ndiyo inacheza mpira, Wazungu wanasema “Money Plays Football” Siku hizi Wazazi Wanaupenda na kuheshimu mchezo huu sababu ya pesa. Ni wazazi Wachache sana wanao wazuia watoto wao kucheza soka.Mbwana Samatta,Mrisho Ngassa na Juma kaseja Wamefanya Wazazi kuwahamasisha Watoto Wao kucheza mpira, Miaka hii ya mpira pesa ukiomba ela kwa ajili ya njumu itawahi kuliko pesa ya daftari na peni,Sammata na gari lake anatafuta wapi pesa zake atawekeza huku engineer mwenye degree yake kila siku kwenye daladala na vyeti akitafuta  ajira.Hiyo ndo Heshima ya soka bwana
 
            Katika miaka ya Karibu Tumeona mabilionea kama Moize Katumbi Chapwe kutoka kongo,Patrice Thopane Motsepe wa South Afika,Said Salim Bakhresa wa Tanzania na wengine wengi wamewekeza zaidi kwenye soka Na kufanya soka letu Afrika liwe La ushindani. Leo hii Teko Modise anaheshimika kuliko Viongozi na watu wengi maharufu wa mjini kwao SOWETO,Tresor Mabi Mputu ndiye mfalme wa KINSHASA,John Boko amekua maarufu kuliko vibopa wa Sinza na kijitonyama,hiyo ndo Heshimi ya pesa za Motsepe ,Bakhresa na Katumbi.
           Lakini kwenye Ulimwengu huu huu wa mpira pesa kuna watu wajanja wajanja,wenye pesa kiasi wanaojua kuwatumia wachezaji kuchota pesa za kina Motsepe,Bakhresa na katumbi.Wengi wao hua wenyeviti au Viongozi wangazi za juu kwenye timu husika. Kule uingereza utamkuta mwenyekiti wa Arsenal,Bwana Peter Hillwood  hakuna arsenal bila hillwood babu yake mzee Samwel Hillwood alikua mwenyekiti wa Arsenal mnamo mwaka 1926-1936 na 1946-1949,pia baba yake mzee Dennis Hillwood alipata kuwa mwenyekiti wa Arsenal mnamo mwaka 1962-1982 kabla ya kufariki na mtoto wake Peter Hillwood kushika hatamu mpaka hivi leo. Peter Hillwood,Ivan Gazids na Mjasiliamali wa kimarekani Stan Kroenke hawa ndo wanaounda CC(Central Comitee) ya Arsenal.
 
Watu hawa wamejaa siasa na roho ya ujasiliamali zaidi,Akili yao yote ipo kwenye kutengeneza pesa kuliko kuimarisha na kujenga timu ya upinzani,Mungu awape nini watu hawa? Wamepata na kocha Mchumi anayejua kucheza na akili ya mashabiki. Profesa Wenger miaka 8 bila kombe ameingiza zaidi ya paund 50 million kama mshahara, Huku akina Piers Morgan na washabiki wenzake wa Arsenal Wakiumia juu ya mwenendo wa timu wa kutoka kapa kila msimu,sambamba na kuuza wachezaji nguli bila kutafuta mbadala sahihi, CC ya Arsenal na  Wenger wao hutazama kwenye zizi na kutafuta kondoo aliyenona kwa ajili ya kuuzwa na mwisho wa mwaka kugawana malupulupu kutokana na faida ya kondoo huyo. Hawa kwa kiasi wameifanya Man City iitwe Man City,wamejua jinsi ya kufyonza pesa za Sheikh Mansour, huku wakiumiza mioyo ya mashabiki wa Arsenal
               

             Hapa kwetu Bongo Yupo fundi aliyepata mafunzo kama ya CC ya arsenal japo kwenye vyuo tofauti. Si mwingine yeye anaitwa Muheshimiwa Aden Rage,mtu huyu amejaaliwa fitina ya soka,siasa pamoja na ujasiriamali. Mashabiki wa msimbazi nikiwauliza mbadala wa Sammata ni nani hawatanipa jibu,Ila Rage kawapa kibuli cha kujisifu kwa kumuuza Sammata kwa mamilioni ya pesa, Hayo mamilioni ya Sammata yameenda wapi? au yameifanyia nini Simba hilo ndo swali la kujiuliza kama mshabiki wa Simba,Vipi kuhusu Ochieng na Okwi?  Kama mmeshindwa kuhoji pesa zilipoenda hojini hata mbadala wa wachezaji hao. Simba Ya sasa inawachezaji wa kawaida na wasio na hadhi ya kuchezea Simba si kwenye mashindano ya kimataifa pekee bali hata ligi ya ndani.

               Sina uhakika kama rage alikua anamtaka Yondani au pesa za usajili za Yondani? Si vibaya Simba kuuza Wachezaji nje ya nchi, ni vizuri sana hasa kwa maendeleo ya soka  letu kwa ujumla, Tatizo lipo kwenye mbadala wa wachezajiwaliouzwa.Leo hii Haruna Chanogo,Singano na Chris Edward wanapewa majukumu makubwa kuzidi umri wao.
               Si lazima uwe mshabiki maarufu wa simba kama Mzee Magoma Moto au Mshabiki Nguli wa Arsenal kama Piers Morgan ili uwe na machungu juu ya kupotea kwa radha kutoka kwenye timu hizi zinazoongozwa na wajasiliamali waliojaa siasa za soka
         
                                 Imeandaliwa na………
kaijage Jr.(Middle Ya Juu)

0 comments:

Post a Comment