Mjumbe wa Bunge la Katiba, Tundu Lissu amesema Tanganyika ilikufa kwa amri iliyotolewa na Mwalimu Julius Nyerere na siyo kwa makubaliano katika hati ya Muungano.
Lissu alitoa kauli hiyo jana alipopata fursa ya
kukamilisha dakika 16 za hotuba yake ya ufafanuzi wa maoni ya walio
wachache iliyokuwa imekatishwa baada ya matangazo ya moja kwa moja ya
Televisheni ya Taifa (TBC1) kukatika Jumamosi iliyopita.
Huku akinukuu maneno yaliyopo katika vitabu
vilivyoandikwa na Profesa Issa Shivji na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa
CCM, Pius Msekwa, Lissu alisema Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila
uhalali wa kisheria kwa kuwa hayakuwapo makubaliano ya kila upande wa
Muungano.
Alisema Aprili 26, 1964 (Siku ya Muungano),
Mwalimu Nyerere alitoa amri ya masharti ya mpito ya mwaka 1964 ambayo
pamoja na mambo mengine iliifuta Tanganyika. Akichambua kitabu cha ‘50
Years of Independence: A Concise Political History of Tanzania’ (Miaka
50 ya Uhuru: Historia fupi ya Tanzania), kilichoandikwa na Msekwa na
kuchapishwa Januari mwaka huu, Lissu alisema:
“Msekwa anasema katika kitabu hicho kuwa amri hiyo
ilichapishwa katika Gazeti la Serikali la siku hiyo. Kwanza,
iliwabadilisha waliokuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika
kuwa watumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”
Alisema hata Mahakama Kuu ya Tanganyika iligeuzwa
kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano na nembo ya Taifa ya Jamhuri ya
Tanganyika iligeuzwa kuwa nembo ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema tarehe hiyohiyo, Mwalimu Nyerere alitoa
amri ya Katiba ya muda ya mwaka 1964 na ilitangaza kuwa Katiba ya
Tanganyika ndiyo iwe Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano.
“Kifungu cha nne cha amri hii ndicho kilichoipatia
Serikali ya Muungano majukumu kuhusu mambo yote ya Muungano katika
Jamhuri ya Muungano yote na vilevile kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano
kwa upande wa Tanganyika,” alisema Lissu huku akishangiliwa na baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo.
Alisema Juni 15, 1964, Mwalimu Nyerere alitoa amri
nyingine iliyoitwa ‘Amri ya Masharti ya Mpito’ ambayo ilieleza kwamba
mahali popote ambako sheria zilizokuwapo zimetaja jina la ‘Tanganyika’
basi jina hilo lifutwe na badala yake jina la ‘Jamhuri ya Muungano’
liwekwe.
Huku akimnukuu Msekwa, Lissu alisema kigogo huyo
wa CCM katika kitabu chake amesema, “Uhai wa Tanganyika ulitolewa kwa
njia hiyo ya amri. Athari za jumla za amri hizi ni kwamba eneo la
kisiasa ambalo ndiyo ilikuwa Tanganyika lilitolewa uhai wake moja kwa
moja kwa amri. Hii ndiyo sababu hata jina la eneo la kijiografia
lililojulikana zamani kama Tanganyika ilibidi libadilishwe na kuwa
Tanzania Bara.”
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Lissu
aliyoitoa jana, Msekwa alisema: “Kitabu kipo na ukikisoma kwa umakini
utagundua kuwa alichokisema Lissu siyo ambacho kimeandikwa. Sasa umhoji
kuhusu hayo aliyoyasema, muulize ameyapata wapi?”
Akimnukuu Profesa Shivji katika kitabu chake ‘Pan Africanism or
Pragmatism? Lessons of Tanganyika – Zanzibar Union’, Lissu alisema
Profesa huyo ameeleza kuwa Muungano huo ulilazimishwa.
“Profesa Shivji amethibitisha kwamba kile
kinachoitwa Sheria ya Kuthibitisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya
mwaka 1964 iliandaliwa na kuandikwa na maofisa wa sheria wa Tanganyika
wakiwa Tanganyika,” alisema.
Alisema kuwa Profesa huyo ameeleza sababu ya
ukweli wa kisiasa uliokuwapo wakati huo ambao Baraza la Mapinduzi kwa
jumla wake halikukaa kuukubali Muungano.
“Profesa Shivji alisema hakuna shaka kwamba
Muungano ‘ulilazimishwa.’ Hivyo, maofisa wa kisheria wa kigeni wa
Serikali ya Tanganyika (waliokuwa pia marafiki wa Nyerere) walitumia
mbinu ya kisheria ya kuchapisha Sheria ya kuthibitisha Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar, mwaka 1964,” alisema huku akikatishwa mara kwa
mara na wajumbe waliokuwa wakiomba miongozo ya mwenyekiti.
“Profesa ameeleza kuwa, kwa sababu utaratibu huo
ulikiukwa, kitendo cha kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika hakikupata baraka za Baraza la Mapinduzi na
kuthibitishwa na kikao halali cha Baraza la Mawaziri la Zanzibar,”
alisema Lissu na kuongeza: “Jamhuri ya Muungano ilizaliwa bila uhalali
wowote wa kisheria kwa maneno ya Profesa Shivji.”
Alisema hata aliyekuwa Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar, Salim Said Rashid kati ya Januari 18 na Juni 1964,
alitamka kuwa:
“Hakuwahi kupokea maagizo kutoka kwa Rais wa
Zanzibar kwa ajili ya kuitisha kikao cha kujadili na kupitisha mkataba
wa kuunganisha Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika,”
alisema Lissu.
Alisema katika kitabu hicho, Profesa Shivji
alieleza jinsi Rashid alivyoeleza utaratibu wa kisheria uliotakiwa
kufuatwa: “... Kwa mujibu wa amri ya mwaka 1964; kila jambo lilitakiwa
kujadiliwa na kikao cha Baraza la Mapinduzi na Mwanasheria Mkuu
kuarifiwa atayarishe ‘presidential decree’ kwa mujibu wa utaratibu.”
Alisema baadaye yeye (Rashid), akiwa Katibu wa
Baraza la Mapinduzi na Baraza la Mawaziri Zanzibar alitakiwa asaini na
kisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na baadaye kutolewa katika
gazeti la Serikali.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kauli hiyo ya Lissu
kuhusu kitabu chake, Profesa Shivji alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno
akisema: “Itakuwa vizuri ukisoma wewe mwenyewe.”
Mbowe: Takwimu za Tume zimetengenezwa na vigogo wa Serikali
Akichangia maoni ya walio wachache kutoka Kamati
Namba Nane, Freeman Mbowe alisema kitendo cha wajumbe wanaotokana na CCM
kubeza takwimu za Tume ya Jaji Joseph Warioba ni kuwakana Watumishi wa
Serikali akisema ilikuwa na watumishi wa Serikali 190 wakiwamo
wanasheria waandamizi.
“Tunapohukumu Tume imefanya kazi chafu ya kuchakachua takwimu
hizi, mjue zimetengenezwa na watumishi waandamizi kutoka Jamhuri ya
Muungano na Serikali ya Zanzibar. Kwa hiyo wanaobeza taarifa ya Tume,
wajue wanaikana Serikali, wanawakana watu ambao wana dhamana ya
kusimamia nchi hii,” alisema na kuongeza:
“Tunapata wapi ujasiri wa kuwadhalilisha wajumbe
wa Tume ya Rais iliyoongozwa na Warioba?... Tume iliyojaa viongozi
walioitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa, tunafanyaje jambo hili?”
Mbowe alisema Jaji Warioba aliwahi kushika
nyadhifa mbalimbali za juu ikiwamo Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa
Rais na kuhoji wajumbe wanapataje ujasiri wa kuwadhalilisha. Aliwataja
wajumbe wengine wa tume hiyo wanaoheshimika kuwa ni pamoja na Jaji Mkuu
mstaafu, Agustino Ramadhan na Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim.
Mbowe pia alishangaa kiwango cha fedha
kilichotumiwa na tume hiyo Sh68.88 bilioni kufanya utafiti ambao leo
wajumbe walio wengi kutoka CCM wanaukana.
Alisema endapo wajumbe wanapuuza msingi wa Rasimu
iliyotokana na Tume ya Jaji Warioba, ni vyema Bunge hilo lisiwepo ili
CCM wakae upya na kutengeneza rasimu wanayoitaka ya serikali mbili.
Alisema Tanzania haiwezi kupata Katiba Mpya kwa uongo na rushwa na
kuzuia watu kujadili kasoro za muungano kwa uhalisia wake.
Jussa awabana mawaziri SMZ
Akitoa ufafanuzi kuhusu maoni ya wajumbe walio
wachache wa Kamati Namba Sita, Ismail Jussa aliwabana mawaziri watatu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwa kushindwa kueleza udhaifu wa
muundo wa serikali mbili bungeni wakati kwenye semina ya Baraza la
Wawakilishi kuhusu mchakato wa katiba walisema hivyo wazi.
Alisema mawaziri hao walilalamikia jinsi wanavyodhalilishwa na muundo wa serikali mbili wanapokwenda nje ya nchi.
“Kuna rekodi hata ya CD, siyo ya Hansard tu
(kumbukumbu rasmi za Bunge), hata ukiitaka mheshimiwa mwenyekiti
nitakupatia. Haya yalikuwa katika semina ya Baraza la Wawakilishi
iliyoitishwa na Spika wetu, Mzee Pandu Ameir Kificho,” alisema.
Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Dk Mwinyi Haji
Makame, Haroun Ally Seleman na Omary Yusuf Mzee. “Walichofanywa Dodoma
sijui mheshimiwa mwenyekiti, lakini wote pamoja na wengine walionyesha
jinsi mfumo huu (serikali mbili) hautusaidii Zanzibar na umetukwamisha,”
alisema.
Alitoa mfano mwingine kuwa kuna siku Zanzibar
walikuwa wakijadili muswada wa utalii ambapo yeye alipendekeza waweke
kipaumbele cha ajira kwa Wazanzibari kwa kuwa wizara hiyo si ya Muungano
na kilikataliwa.
“Mimi na Asha Bakari tu wa CCM tulitoka nje na
akalalamika kuwa wenzake wamemgeuka. Kwa tabia hii mheshimiwa mwenyekiti
tunapokuwa Zanzibar, tunasema wengine tunapokuja Dodoma tunaufyata,
Wazanzibari watatuhukumu,” alisema.
Awali akisoma maoni ya walio wengi, Mwenyekiti wa Kamati Namba
Sita, Stephen Wassira alisema walio wengi walipendekeza muundo wa
serikali mbili kwa sababu unatoa fursa kubwa ya kisiasa, kiuchumi na
kijamii kwa pande zote mbili na kuondoa tabaka la ukabila na udini ndani
ya Jamhuri.
“Mfumo wa serikali mbili ukifanyiwa marekebisho ya
kikatiba utaondoa kero na manung’uniko ambayo yameelezwa kuwa msingi wa
mapendekezo ya Tume ya kutaka mfumo wa serikali tatu,” alisema.
Imeandaliwa na..........
Katemi Methsela
Imeandaliwa na..........
Katemi Methsela
0 comments:
Post a Comment