Uharibifu wa barabara uliotokana na mvua zinazoendelea kunyesha, umeendelea kuwatesa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa mbalimbali nchini hasa baada ya mabasi ya mikoani kuzuiwa kufanya safari zake jana.
Amri ya kuzuia mabasi hayo ilitolewa jana ikiagiza
mabasi yote yasiondoke katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo hadi
itakapotangazwa vinginevyo, kutokana na uharibifu wa Barabara za Kilwa,
Morogoro na Bagamoyo ambako madaraja yamevunjika.
Dereva wa Basi la Adventure liendalo Kigoma,
Joseph Luciano alisema walitangaziwa na Sumatra na trafiki kuwa wasubiri
mpaka hapo watakapojulishwa kuondoka.
“Hatuwezi kuondoka mpaka Serikali itakapotangaza
ili kuepuka faini ambayo wenzetu, wale wanaopakia nje, wametozwa,”
aliongeza huku ikielezwa kuwa baadhi ya mabasi yalitozwa faini kwa
kukiuka amri hiyo.
Abiria anayesafiri kwenda Kibondo, Kigoma, Lydia
Lutakinikwa alisema: “Nilikuja kuchukua mzigo wa duka langu tangu Ijumaa
na nimekuwa nikilala gesti. Nimeishiwa hela hivyo nalazimika kuendelea
kuwapo kwenye hili basi kwa kuwa sina tena pesa ya kwenda kulipia
malazi.”
Kondakta wa Basi la Taqwa liendalo Nairobi, Yahaya
Maulid alisema wameruhusu kubadilishwa tiketi za abiria wao, kama
walivyoelekezwa na mamlaka husika ili kutoa nafasi kwao kujipanga upya.
Mkuu wa Usalama Barabarani Ubungo, Inspekta wa
Polisi, Yusuf Kamutta alisema zaidi ya mabasi 400 yameathiriwa na uamuzi
huo... “Tumezuia mawakala wasitoe tiketi mpya kwa sababu abiria wa leo
(jana) ndiyo wanaotarajiwa kusafiri kesho, hivyo wanaweza kuuza tiketi
za kuanzia keshokutwa.”
Msururu wa magari Pwani
Kutokana na kuharibika kwa baadhi ya madaraja
katika Mkoa wa Pwani, magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka maeneo
mbalimbali yalikwama katika maeneo tofauti. Baadhi yalikwama Visiga na
mengine Mlandizi jirani na Kituo cha Polisi katika misururu mirefu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei
aliwataka wamiliki wa magari makubwa ya mizigo wanaotumia barabara hiyo
kusitisha safari zao kwa kipindi hiki hadi hapo hali itakapotengamaa.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani na
uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ililazimika kuweka
kambi kwa siku nzima eneo la Mlandizi jirani na daraja la Ruvu kusimamia
shughuli ya ukarabati wa daraja dogo lililokuwa na hitilafu.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Tumaini
Sarakikya alisema hadi jana mchana magari yalikuwa yameanza kupita
upande mmoja, lakini baadaye jioni yangeanza kupita bila wasiwasi.
0 comments:
Post a Comment