Facebook

Tuesday 22 September 2015

Makanisa matatu ya kilokole yachomwa moto Bukoba.

Makanisa matatu ya dhehebu la Kipentekoste yaliyopo katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, yameteketezwa kwa moto usiku wa kuamkia leo na watu wasiofahamika.
Tukio hilo limehusisha makanisa ya Pentecostal Assemblies of God (PAG) lililopo Buyekera Kata ya Bakoba, Living Water International na Evangelical Assemblies of God (EAGT) yote yakiwa eneo la Kashura.
Akizungumzia tukio hilo Mchungaji wa Kanisa la EAGT, Athanas, amesema saa 10 alfajiri alipigiwa simu na jirani yake na kuelezwa kanisa linaungua moto na kumfanya kukimbia kwenda eneo la tukio.
Mchungaji Athanas amesema baada ya kufika eneo la tukio alikuta moto mkubwa ambao usingeweza kuzimwa kwa kumwagia maji, hali iliyosababisha vitu vyote vilivyokuwa ndani ya kanisa hilo kuteketea ikiwa pamoja na viti 60, meza, mabenchi, vifaa vya ujenzi na madhabahu.
Amesema hawajafahamu watu waliohusika na tukio hilo, lakini alidai waliponusa baadhi ya vitu walisikia harufu ya mafuta ya taa hali iliyopelekea wahisi wachomaji walitumia mafuta ya taa kuteketeza kanisa hilo.
Mchungaji huyo alisema hilo ni tukio la tatu la makanisa ya EAGT kuchomwa moto, wakati mara ya kwanza ilikuwa Septemba 2013 na kufuatia lile la Aprili mwaka jana.
Naye Mchungaji Alistides Kabonaki wa kanisa la Pentekoste P.A.G, alisema saa 11.50 asubuhi jana, aliitwa na msichana wake wa kazi na kumweleza kuna moto unawaka kanisani.
Kabonaki alisema kanisa lote limeteketea pamoja na mali zilizokuwamo ndani huku waliohusika na tukio hilo akiwa hawafahamu walikuwa na lengo gani.
Amesema alitoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa pamoja na polisi, hivyo kwa sasa anasubiri hatua za kiuchunguzi za jeshi hilo ili kubaini waliohusika na sababu za kufanya hivyo.
Mchungaji huyo alisema kabla ya uchomaji wa kanisa hilo, watu hao wasiofahamika walivamia kanisa lao na kuiba baadhi ya mali zilizokuwamo ikiwamo viti na vitambaa vya madhabahu.
Akizungumzia tukio hilo, Regina Bakera, ambaye ni jirani na kanisa la PAG, alisema kama muumini amesikitishwa na matukio hayo na hawafahamu waliosababisha hilo.
Bakera alisema matukio hayo yanadhihirisha kuna kikundi kilichoandaliwa kwa ajili ya kuchoma makanisa na kuiomba serikali kuyashughulikia kufanya upelelezi wa kina.
Kufuatia uchomaji wa makanisa hayo, umoja wa wachungaji katika mkoa wa Kagera, umepanga kufanya maandamano ya kulaani kitendo hicho mkoa mzima maana serikali ilishindwa kutatua matatizo yanayowakabili ikiwamo la makanisa yao kuchomwa moto.
Mwenyekiti wa Makanisa hayo mkoa wa Kagera, Crodward Edward, alisema kwa sasa wanachukua hatua ya kujilinda kwa sababu serikali ilishindwa kufanya hivyo pamoja na vikao ambavyo wamekaa viongozi wa serikali na viongozi wa makanisa hayo.
Akizungumzia matukio hayo amesema siku za nyuma yalichomwa makanisa saba katika mkoa wa Kagera huku moja likihusisha pia mauaji ya muumini mmoja na waliokamatwa wakiachiwa huru bila kuelezwa kinachoendelea na sasa yamechomwa matatu kwa siku moja.
Naye Mchungaji Aneth Sebastian ambaye ni Katibu wa wachungaji katika manispaa ya Bukoba alisema sasa wanashindwa kuiamini serikali na polisi kwa sababu watakuwa wanawafahamu wanaohusika na vitendo hivyo bali wanawakingia kifua.
Tathmini ya hasara iliyotokana na uchomaji wa makanisa hayo ambayo mawili yameteketea kabisa bado inaendelea, ili kujua hasara iliyotokana na uchomaji moto huo.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, alisema kwa sasa yuko safarini na atatoa ufafanuzi kuhusiana na tukio hilo baadae

0 comments:

Post a Comment