Facebook

Friday 18 September 2015

Kila Chama kupata Sh 17 Bilioni za Uchaguzi Mkuu 2015.

Dar es Salaam. Serikali imetoa waraka unaotokana na sheria ya gharama za uchaguzi unaokitaka kila chama cha siasa kutumia kiwango kisichozidi Sh17 bilioni katika kampeni zake za uchaguzi wa Rais na wabunge.
Waraka huo uliomo kwenye Tangazo la Serikali Namba 325 la Agosti 18, lililo na kichwa kisemacho “Amri ya Gharama za Uchaguzi Mwaka 2015”, limesainiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Ofisa habari wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Monica Laurent alisema ofisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ndio wenye jukumu la kufuatilia iwapo wagombea hao wanafuata sheria hiyo nchini kote.
“Kuna timu ya watu ambayo iko katika maeneo mbalimbali nchini inafuatilia matumizi na gharama za uchaguzi,” alisema.
Alisema matumizi ya fedha zilizoanishwa yakizidi, wagombea watakuwa wamevunja sheria hiyo na hatua zitachukuliwa.
Mwanasheria wa ofisi hiyo, Piencia Kiure alisema utekelezaji wa sheria hiyo utaangaliwa hata kama mgombea atakuwa ameshinda au kushindwa.
“Kama umevunja sheria ya gharama za uchaguzi, hatua za kisheria zitachukuliwa bila kujali kama ulishinda katika uchaguzi au umeshindwa,” alisema.
Akizungumzia gharama hizo mjumbe wa kampeni za CCM, January Makamba alisema gharama za chama chao hazitafika huko kwa kuwa sheria hiyo ilitungwa na Serikali ya CCM, hivyo ni lazima waiheshimu.
Alisema sheria hiyo ya kudhibiti gharama ni nzuri na pia inadhibiti kuingizwa kwa fedha chafu kwenye uchaguzi.
Profesa Prosper Ngowi wa Chuo Kikuu Mzumbe aliyejikita kwenye masuala ya uchumi, alisema kiwango hicho cha fedha kilichowekwa na sheria ni kikubwa, lakini inategemea kila chama kinataka kuzitumia kwa kazi gani.
Mathalan, alisema kama chama kinategemea kutumia usafiri wa basi na magari, kwa vyovyote fedha hizo haziwezi kuisha, lakini hali itakuwa tofauti kama wanatumia helikopta na matangazo makubwa.
Hata hivyo, Profesa Ngowi alisema hadhani kama kuna utaratibu wa kusimamia vizuri utekelezaji wa sheria hiyo.
Katika mchanganuo wa gharama hizo, majimbo ya ubunge yamepangiwa gharama tofauti kulingana na vigezo mbalimbali vikiwamo ukubwa na changamoto za kila eneo.
Katika ukurasa wa 23, sehemu ya tatu, waraka huo unaonyesha kuwa kiasi hicho ni cha juu kinachoweza kutumiwa na chama cha siasa kwenye kampeni za uchaguzi kuanzia mchakato wa uteuzi wa wagombea udiwani, ubunge na urais hadi uchaguzi wenyewe.
Waraka huo unaonyesha kwamba mgombea urais wa chama atatakiwa kutumia kiasi kisichozidi Sh6 bilioni.
Sheria hiyo inaeleza kuwa madiwani wanaogombea katika kata za mijini watatakiwa kutumia kiasi kisichozidi Sh8 milioni wakati wale wa vijijini wanatakiwa kutumia kiasi kisichozidi Sh6 milioni tu.
Kwenye kampeni za uchaguzi, vyama hutumia fedha nyingi katika usafirishaji wa wagombea, hasa wa urais kwenye mikoa mbalimbali, uchapishaji mabango ya matangazo, malipo ya mawakala, malipo ya matangazo ya redio na televisheni, usafirishaji wa timu za kampeni, malazi yao na posho na gharama nyingine.
“Lengo la sheria hiyo ni kuhakikisha vyama vya siasa vinaendana na gharama za uchaguzi,” alisema kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.
Katika sheria hiyo, majimbo 267 ya Tanzania yamegawanywa katika makundi sita yanayoainisha gharama za majimbo ambazo zinaanzia Sh33 milioni hadi Sh88 milioni.
Sheria hiyo inasema upangaji wa viwango hivyo umezingatia tofauti ya ukubwa wa jimbo, idadi ya watu katika jimbo na miundombinu ya mawasiliano ndani ya jimbo la uchaguzi.
Baadhi ya majimbo yaliyo katika kundi la kwanza lenye gharama ambazo hazitakiwi kuzidi Sh33 milioni ni Ilala, Magogoni, Chakechake, Konde na Kojani.
Katika kundi la pili baadhi ya majimbo ambayo gharama zake hazitakiwa kuzidi Sh44 milioni ni Chilonwa, Kibakwe, Mpwapwa, Gairo, Mufindi na Makete.
Sheria hiyo inaainisha kuwa kundi la tatu ambalo gharama za uchaguzi kwa wabunge hazitakiwa kuzidi Sh55 milioni. Baadhi ya majimbo hayo ni Mtera, Chemba, Ukonga, Igalula, Urambo na Segerea.
Sheria hiyo inaonyesha kundi la nne limepangiwa kiasi kisichozidi Sh66 milioni ambazo zitatumiwa na wabunge.
Baadhi ya majimbo hayo ni Bahi, Kondoa, Kongwa, Muhambwe, Rufiji, Chato na Lulindi.
Katika waraka kundi la tano limepangiwa kiasi kisichozidi Sh77 milioni ambazo zitatumika kwenye mchakato wa kugombea ubunge. Baadhi ya majimbo katika kundi hilo ni Mbarali, Handeni Vijijini, Kigamboni, Kinondoni, Katavi na Mbinga.
Katika sheria hiyo Kundi la sita limepangiwa kiasi kisichozidi Sh88 milioni na baadhi majimbo yananayoangukia kwenye kiasi hicho cha fedha ni Igunga, Ubungo, Temeke, Kilombero, Kahama, Kibamba, Ushetu na Bariadi
“Fedha za ziada ambazo zinaweza kutumiwa katika mazingira maalumu kama gharama za uchaguzi, hazitatakiwa kuzidi asilimia 15 ya gharama ya kiasi halisi cha fedha kilichoanishwa katika jedwali,” unaeleza waraka hiyo.

CHANZO:MWANANCHI.

0 comments:

Post a Comment