Facebook

Saturday 19 September 2015

Wakenya 3 wauawa kwa Ujambazi Arusha.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas Arusha amesema Majambazi wane, wakiwemo raia watatu wa Kenya wameuwa na polisi mkoani Arusha baada ya kuhusika kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi wa kupora silaha pamoja na fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Kamanda wa polisi, Liberatus Sabas amesema kuwa majambazi  waliouwawa watatu ni raia wa Kenya ambapo bado majina yao kamili hayajajulikana huku raia wa Tanzania ametambulika kwa jina la Sixtus Alfredy.

Kamanda Sabas amesema kuwa ,polisi walianza kujibu majibizano hayo ndipo walipofanikiwa kuua majambazi watatu ambao walikutwa na vitambulisho vitatu vya Jamhuri ya Kenya vyenye majina ya Simon Githinji Kariuki,Bonifas Mwanmgi Mbulu, Thadeo Kamau Njuguna na kitambulisho kimoja cha UN-ICTR chenye jina la Chacha John Marwa.
Vitambulisho vingine walivyokutwa navyo ni leseni ya udereva iliyotolewa Kenya yenye jina la Thadeo Kamau Njuguna , kadi ya Benki ya Equity Master Card yenye jina la Simon Githinji pamoja na kadi ya Benki ya Cooperative yenye jina la Thadeo Kamau Njuguna , simu tano aina ya Nokia , Tecno na Sumsung.

Amesema kuwa, majambazi hao watatu kila mmoja alikutwa na bastola pamoja na risasi , mabegi matatu meusi ambapo baada ya kuyafungua walikuta bunduki aina ya AK 47 mbili, SMG moja, bastola tatu, magazine nne za SMSg, risasi 85 za SMG na AK 47 na risasi nyingine 28 za bastola.

Kamanda Sabas amesema kuwa, tukio hilo lilitokea jana Septemba 17 mwaka huu majira ya saa 3:30 usiku katika maeneo ya Chekereni wilayani Arumeru ambapo polisi walipata taarifa za kiintelejensia toka Agosti 19 mwaka huu juu ya kuwepo kwa kundi la majambazi wanaotoka nchi jirani ya Kenya na kuja hapa nchini kwa nia ya kufanya uporaji kwa kushirikiana na majambazi wenzao wa hapa nchini.

Alisema miili ya marehemu wote imehifadhiwa katika Hopsitali ya Mkoa ya Mount Meru huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi zaidi wa kuwatafuta watuhimiwa wengine waliotoroka katika tukio hilo na kubaini mtandao wa majambazi hao.

CHANZO:MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment