Facebook

Sunday 1 March 2015

Simba yazinduka taifa na kushusha kipigo kizito kwa Prisons.

Wekundu wa Msimbazi Simba SC imefanikiwa kurejesha heshima na kutuliza nyoyo za mashabiki wake baada ya kuitungua Tanzania Prisons jumla ya mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa katika dimba la taifa jijini Dar es salaam.

Mabao ya Simba yamefungwa na Ibrahim Hajib aliyefunga mabao matatu katika dakika za 15, 21 na 42. Bao la nne limefungwa na Emanuel Okwi dakika ya 73 na Ramadhani Singano ‘Messi’ dakika 83.
Ushindi huu umetuliza nyoyo za mashabiki na wanachama wa Simba ambayo kesho (Jumapili Machi 1) itafanya mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo.
Wakati huo huo Simba imepata pigo lingine kwa kuondokewa na mchezaji wao wa zamani Zuberi Magoha aliyefariki na kuzikwa leo jijini Dar es salaam.
Mjini Shinyanga pambano kati ya Stand United na Kagera Sugar limevunjika kutokana na mvua kubwa kunyesha na kusababisha uwanja wa Kambarage kujaa maji hali iliyosababisha mwamuzi kuahirisha mchezo katika dakika ya 80.

Wakati mchezo huo unaahirishwa, Stand United ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Mnigeria Abaslim Chidiabele kwa njia ya penati baada ya yeye mwenyewe kuchezewa madhambi katika dakika ya 45.
Mchezo huo utarudiwa kesho asubuhi kwa dakika 10 zilizobaki.
Matokeo mengine ni kwamba Coastal Union imeifunga Mgambo JKT 1-0 lililofungwa na Mganda Yayo Lutimba katika dakika ya 88.

Mkoani Mbeya Timu ya Mbeya City imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting.
Kwa matokeo haya Simba imefikisha point 23 nafasi ya 4 sawa na Ruvu Shooting huku Coastal Union ikifikisha point 22 nafasi ya 6, Mbeya City point 18 nafasi ya 12, Mgambo imebaki katika nafasi ya 13 ikiwa na point 17 na Prisons nafasi ya 14 (mkiani) ikiwa na point 12.

0 comments:

Post a Comment