Facebook

Friday 20 March 2015

Zitto Kwabwe abwaga manyanga rasmi,hii ndiyo hotuba yake aliyotaka kuitoa jana Bungeni.

Hotuba ambayo Zitto kabwe alikusudia kuitoa Bungeni tarehe 19 March 2015.

Mheshimiwa Spika, nilijiunga na Bunge
lako tukufu mwaka 2005 nikiwa kijana
mdogo mwenye malengo ya kupaza
sauti ya vijana kwenye masuala
yanayohusu nchi yetu na pia kutetea
maslahi ya wananchi wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma.
Katika kudumu kwangu kama mbunge
nililelewa na kukuzwa na chama cha
siasa cha CHADEMA ambacho kupitia
chama hiki niliingia Bungeni. Chama
hiki kilinilea na kunikuza tangu nikiwa
na umri wa miaka 16 na kupitia chama
hiki nimejifunza mambo mengi sana.
Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na
nimejulikana ndani na nje ya nchi.
Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipotoa
shukrani zangu za dhati kabisa kwa
CHADEMA na viongozi ambao
nimefanya nao kazi muda wote nikiwa
mwanachama na kiongozi.

Mheshimiwa Spika, Chama kilinikuza
kama mwanasiasa lakini watu wa
Kigoma Kaskazini ndio walionipa kiti
hiki ninachokalia kama Mbunge. Juzi
nilipokuwa nyumbani nilipata fursa ya
kuwashukuru rasmi wananchi kwa
imani waliyonipa kuwatumikia kwa
vipindi viwili mfululizo. Wengi wenu
ndugu zangu wabunge mnafahamu,
mihula miwili sio jambo la mchezo, sio
lelemama. Mola atawalipa wananchi wa
Kigoma kwa imani kubwa
walioionyesha kwangu na kuniwezesha
kulitumikia Taifa langu kwa namna
nilivyolitumikia.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii
leo kuzungumzia suala la muda mrefu
sasa la kutoelewana kati yangu na
chama changu na hivyo kuleta
msuguano kati ya wananchi
walionichagua kuwawakilisha na
chama nilichopitia na kupeperusha
bendera yake wakati wa uchaguzi
mkuu. Licha ya msimamo wangu wa
siku zote kwamba wananchi pekee
waliomchagua mwakilishi wao ndio
wawe na mamlaka ya kumwondoa
kwenye uwakilishi mchaguliwa huyo,
mfumo wetu wa kikatiba na mfumo
wetu wa kisiasa haupo hivyo na
umeamua vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, kwamba chama
cha siasa kinaweza kumvua
uanachama mwanachama wake na
hivyo kupoteza kiti chake cha
uwakilishi wa wananchi wake ni moja
ya makosa makubwa ya kikatiba
ambayo tumeendelea kuyakumbatia,
nimekuwa nikipinga na nitaendelea
kupinga udikteta wa vyama dhidi ya
utashi wa wananchi.

Mheshimiwa Spika, licha ya upinzani
wangu mkali wa vifungu kandamizi vya
kikatiba, kama mzalendo ninaiheshimu
Katiba yetu na mfumo wetu wa sasa na
ninaheshimu uamuzi wa mahakama
dhidi ya kesi yangu na sitakata rufaa.
Hatua itakayofuata ni uamuzi wa
chama changu na baadhi ya viongozi
wameshatangaza kwa umma kupitia
vyombo vya habari kunivua
uanachama ingawa sijapewa taarifa
rasmi.

Mheshimiwa Spika, ningeweza kukata
rufaa kuhusu maamuzi ya mahakama
kwani kuna sababu lukuki ya kushinda
rufaa hiyo. Lakini ninadhani
nimepigania haki zangu kwa muda
mrefu sasa. Nimepigania kupanua wigo
wa demokrasia ndani ya chama
changu kwa muda mrefu sasa. Lakini
ugomvi huu hauna manufaa kwa pande
zote husika, kwa hakika unatuumiza
wote. Mimi ni mwanademokrasia.
Naamini katika siasa za ushindani
ndani ya chama na katika mfumo
mzima wa siasa kitaifa. Lakini
sitakuwa tayari kudhoofisha harakati
na kazi kubwa walizofanya
wanamageuzi waliotutangulia kwa
kuendeleza ugomvi unaotuumiza.

Hivyo niko tayari kukubali kukaa
pembeni. Ninaamini kuwa mapambano
ya kuleta mabadiliko ya kweli na
demokrasia katika nchi yetu Tanzania
ni makubwa kuliko mimi, kuliko
kiongozi yoyote wa Chadema na kuliko
wanachama wa Chadema. Mapambano
haya ya mabadiliko si kwa ajili ya
kizazi hiki tu bali kwa vizazi vijavyo.
Ndiyo maana siku zote nimesema Nchi
kwanza, vyama baadae. Kuona
makundi yanajitokeza ndani ya
harakati hizi, na kuwa na uhasama
mkubwa uliopindukia, unawakatisha
tamaa wananchi wanaotutumaini kuleta
siasa iliyo tofauti na siasa za sasa.
Muda umefika wa kupiga mstari na
kuanza upya. Hivyo nimeamua kuwa
nitatii maamuzi ya chama ya kunivua
uanachama na kung’atuka ubunge.

Mheshimiwa Spika, naomba niweke
wazi kuwa nimefikia uamuzi huu kwa
utashi wangu mwenyewe na nimepewa
Baraka zote na wananchi wangu na
wazee wa Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Najua Watanzania wengi ambao
nimewatumikia kwa moyo wangu wote
katika kipindi cha miaka hii 10
wanaweza wasikubaliane na uamuzi
huu. Hata hivyo Watanzania wajue
kuwa mfumo wetu wa siasa na katiba
unatoa nguvu kwa vyama vya siasa
kudhibiti wabunge wake. Naamua hivi
kwa sababu wenzangu ndani ya chama
ambao nimehangaika nao usiku na
mchana kujenga chama na kukifisha
hapa kilipo hawapo tayari kufanya kazi
tena na mimi. Nimesoma na kusikia
kauli nyingi zinazoweka wazi kuwa
hawanitaki ndani ya chama.
Nimejitahidi kwa njia zangu zote kuona
kama tunaweza kuendelea kufanya
kazi pamoja ya kujenga mfumo
madhubuti wa vyama vingi nchini lakini
imekuwa ngumu kama mwanachama
mwenzao. Ninaheshimu uamuzi wao
huo.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi hii
si yote niliyafanya sahihi, yapo ambayo
niliyakosea kama mwanadamu katika
kufanya kazi kwangu, kwa namna
yeyote ile naomba radhi Watanzania
wote kwa yote ambayo sikuyafanya
kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe
dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake
amekamilika.
Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza
maisha yangu mapya bila ya
kulishukuru Bunge lako tukufu, Bunge
la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta na
Bunge la Kumi chini yako Mama Anna
Simamba Makinda. Bunge limekuwa ni
nyumbani kwangu kwa takribani
muongo mmoja. Nimekuzwa,
nimejifunza, nimepambana, nimefurahi
na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa
pamoja tumepigania maslahi ya
wananchi wetu na kupingana na
kufanya mambo kwa mazoea na hivyo
kuleta mabadiliko kadhaa. Ni kipindi
hiki ambapo wabunge tumekuwa na
sauti, Bunge la Tisa lilijenga ‘Bunge
lenye Meno’ katika kupambana na
ufisadi. Bunge la Kumi limejenga
‘Bunge lenye nguvu’ katika mfumo wa
Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili
tumeweka misingi ya kujenga mfumo
madhubuti wa uwajibikaji katika nchi
yetu.
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la
Tisa litakumbukwa kwa hoja ya
Buzwagi iliyopelekea nchi yetu kufanya
mabadiliko makubwa katika mfumo wa
uendeshaji wa sekta ya madini (Sera
mpya ya Madini na Sheria mpya ya
Madini ) na hivyo mapato ya sekta ya
madini kuongezeka kutoka Tshs 32
bilioni kwa mwaka mpaka Tshs 450
bilioni kwa mwaka hivi sasa; Bunge la
Kumi litakumbukwa kwa hoja maalumu
ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo
wetu wa maadili ya Viongozi kupitia
Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi
kwa namna ambayo haijawahi
kushuhudiwa katika miaka iliyopita.
Mimi kuwa sehemu ya mabunge
yaliyotekeleza hatua hizo za
mabadiliko ni jambo la kujivunia sana.
Mheshimiwa Spika, kwa familia yangu,
wajumbe wa PAC, tumekuwa nguzo
kubwa ya kujenga uwajibikaji wa
Serikali kwa Bunge na wananchi.
Napenda kuwashukuru kwa dhati
kabisa kwa kuniunga mkono na kwa
kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti
wao. Changamoto na malezi mliyonipa
kwa miaka yote hii yamejenga
Mtanzania mmoja mwenye dhati ya
kuitumikia nchi yake, muda wowote,
wakati wowote na kwa namna yeyote
ile bila woga wala upendeleo.
Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa
nchi yetu na dhamira isiyo na mawaa
ya kujenga Taifa imara zaidi.
Nitaendelea kuwatumikia wananchi wa
Kigoma Kaskazini na Taifa langu hata
kama nimelazimika kuachia nafasi
yangu ya ubunge kwa kipindi hiki
kilichosalia kwa kusimamia ukweli,
kutetea demokrasia ya kweli na
kupigania maendeleo ya kweli kwa
mwananchi wa kawaida bila ubaguzi
wowote.
Mheshimiwa Spika, Kwa CHADEMA,
licha ya tofauti zetu ambazo zimekua
kiwango cha kutosameheka, najivunia
kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya
Baraza hili la Taifa ambalo leo
ninalihutubia kwa mara ya mwisho
kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Fursa iliyonifanya niweze kuitumikia
nchi yangu na mkoa wangu wa
Kigoma. Inawezekana tusiweze
kuelewana katika masuala ya uongozi,
misingi na itikadi, lakini ninaamini
tunapaswa kuelewana na kukubaliana
katika kubwa ya kuijenga nchi yetu
kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo na
aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye
uchumi shirikishi wenye kuzalisha ajira
na kuondoa umasikini, ujinga na
maradhi, Taifa la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Na ni
matumaini yangu kuwa tutakuwa bega
kwa bega katika harakati hizi katika
siku zijazo. Yaliyopita si ndwele
tugange yajayo, nafasi hii ya kihistoria
tuliyopewa haihitaji siasa za ubinafsi na
unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa
uwezo wetu wa kuweka tofauti zetu
binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa
zaidi yetu.
Mheshimiwa Spika, Mwisho kwa
wananchi wa Jimbo langu, wana
Kigoma na raia wote wa Tanzania
ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika
viti hivi kwa miaka takribani kumi,
nawahakikishia kuwa dhamira yangu
kuwatumikia, nia yangu na sababu za
kutoa utumishi wangu kwenu
vimekuwa na nguvu zaidi kuliko wakati
mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo
mpya. Ngugi aliandika ‘a grain of
wheat’ kwa maana ya kwamba ‘Ili
Mbegu iweze kumea lazima ife
kwanza’.

Asanteni sana.

0 comments:

Post a Comment