Facebook

Saturday 23 May 2015

KWAHERI STEVEN GERRARD CAPTAIN FANTASTIC , HASTA LA VICTORIA SIEMPRE

Usiku wa tarehe 23 April 2003, ni usiku ambao kaka yangu kipenzi, na shabiki mkubwa wa Manchester United Nelson aliamini Real Madrid walikuwa wanaenda kuchukua ubingwa wa ulaya kwa mara nyingine. Katika uwanja wa Old Trafford Ronaldo De Lima anafunga hattrick, kwa mara ya kwanza tangu 1992 Old Trafford mchezaji wa timu pinzani anafunga magoli matatu na wakati anafanyiwa mabadiliko uwanja mzima unanyanyuka kumpigia makofi. Ndio ilikuwa mechi ambayo Ferguson aliomba Raul ambaye alikuwa amefunga magoli mawili mechi ya kwanza Santiago Bernabeu asicheze na maombi yake yakajibiwa, ikawa kama aliomba gharika. Kila jicho lilikuwa linashuhudia kipaji bora kabisa ambacho Pamoja na kuandamwa na majeruhi yalipitiliza alibakia Kuwa mshabuliaji aliyekamilika zaidi kuwahi kuukanyaga uso wa dunia hii achilia mbali kikosi kile cha Madrid ambacho bado naamini wanaota kukipata. Ile ndo ilikuwa Galactico achana na hii ambayo hata James Rodriguez imemgeuza moja ya wachezaji bora kabisa ulimwenguni . Kama Kuna mtu alipelekwa jela siku hiyo na akatoka Leo, hawezi kukubali jambo moja tu,  Kuwa Ronaldo De Lima hakushinda taji la ulaya, achilia mbali ubora wake bali pia kilikuwa ni kikosi cha Madrid ambacho ungejaribu kukiwekea uhai wako kwa pesa na bado ukawa una imani wewe ndo una nafuu kuliko aliyeweka pesa. Lakini ndivyo maisha yalivyo mkono wa De Lima ulibaki kuwasha bila Majibu. Ni kama pale Uingereza kwa mtu yoyote katika utimamu wa kawaida timilifu kujaribu kujiuliza sababu Za Gerrard kutokushinda kikombe cha ligi chochote ama ligi yoyote kubwa. Mchezaji ambaye kila mboni ilistaajabu uwezo wa miguu yake,  mchezaji ambaye busara Za Zinedine Zidane ziliamini alitakiwa kushinda japo mara moja mchezaji bora wa dunia. Hakuwahi, hajaweza na pengine hatofanikiwa kushinda taji la ligi kuu. Kuna mambo mawili tu yatakuja kichwani kwa shabiki asiye wa Liverpool, ataamini ni Utii wake kwa Liverpool ndo ulimponza, pia Liverpool haikumtendea haki kwa Muda mrefu. Ametembea miaka mingi akiwa Handicapped (akiipambania Liverpool iliyokuwa dhaifu) katika mazingira magumu na dhidi ya timu ngumu hasa,  aliifanya Liverpool yenye Djibril Cisse kuonekana tishio, alifanya fainali ya Instabul kuishi daima mioyoni na machoni pa watu, aliifanya fainali dhidi ya West Ham FA kubaki vitabuni kwa Liverpool. Kifupi alifanya kila kobe Liverpool aonekane Duma na kila mbilikimo aonekane Twiga.

Katika dunia Kuna mfululizo wa matukio ya ajabu, ambayo yakizoeleka yanaonekana ya kawaida. Ni kama la Gerrard. Ni tukio la ajabu lakini linalojaribu kuzoeleka, limezungumzwa likakubalika, limefichwa likafichika Kisha likaaminika. Hakuna tusi kali kwa mashabiki wa Liverpool kama kusema Gerrard hajashinda taji la ligi kuu. Kwao Ile miaka 25 bila kombe inavumilika kuliko huyu kutokuwa na kombe. Wanatamani angekuwa kizazi cha mwisho cha John Barnes wakati wanashinda. Lakini ndiko mshale wa saa ulikowapeleka, timu haijashinda kombe kwa miaka 25, na kijana wao mtiifu kabisa anaondoka. Hakuna siri inayowatesa kama Ile ya Kuwa hawatompata Gerrard mwingine katika akina Raheem Sterling walionao. Hakuna kidonda kibaya kama kile cha nafasi ya Gerrard itatumiwa na Jordan Henderson kwa kiasi kikubwa. Ajabu ya yote ni Ile namba 8, mgongo pekee unaotakiwa kubeba Ile namba kwa sasa ni sanamu ya Gerrard Liverpool. Kuibeba jezi Ile ni kama kujaribu kuvaa viatu vya Ferguson katika Ulimwengu huu pale Manchester United . Hii ndo zawadi pekee ambayo nafikiri inamfaa Steven Gerrard, hakuna kingine. Bahati nzuri amekuwa kijana mtiifu kiasi cha kuficha machozi yake siku ya kuagwa. Machozi pekee aliyatoa dhidi ya Man City April 13 2014, yale yaliambatana na ukweli kwamba aliona ndoto yake ikielekea kutimia kama sio vile viatu alivyovyaa dhidi ya Chelsea kumwangusha. Huyu ndiye mwanamapinduzi pekee ambaye aliweka imani Za mashabiki wa Liverpool juu. Alifanikiwa kila sehemu isipokuwa hapo tu. Kuna siku niliandika makala nakisubiri kitabu cha Steven Gerrard, acha niendelee kukisubiri,  nawaza Jina lake,  nawaza atasema nini. Lakini nina hamu ya kusoma kipande cha ubingwa wa ligi kuu,  natamani auseme ukweli utakaouma. Ule wa Kuwa anajutia kutokuondoka kama Alonso,  ule wa kusema katika maisha yake ni mara moja tu aliwahi Kuwa na kikosi sahihi kile cha Mascherano, Alonso na Torres kabla hakijasambaratika,  ukweli wa Kuwa aliipa Liverpool kila inachotaka lakini mara nyingi haikujibu fadhila. Kuanzia kwa wamiliki George Gillet na Thom Hicks mpaka hawa FSG akina John Henry. Wote hawakumtendea haki kijana mtiifu huyu. Ni kama ambavyo najaribu kuwaza watakavyojaribu kumpa Joe Allen urithi wa Ile jezi, umefika wakati kama hawakuheshimu uwepo wake itabidi waheshimu jezi yake.

Mwanaharakati na mwanamapinduzi Ernesto Che Guevara, baada ya kuwasaidia Cuba kupata uhuru wa mapinduzi aliona bado ana kazi kubwa ya kufanya,  alihisi dunia bado inamdai, alijua bado anatakiwa kufanya sehemu nyingine. Kwake nchi kama Congo Brazzaville zilitakiwa Kuwa huru, nchi kama Bolivia ambayo ndiko alikouawa zilitakiwa Kuwa na uhuru. Alienda huko kufanya kazi kama ya Gerrard, kutembea akiamini yeye ndo kiongozi, yeye ndo mwenye mbinu, hakuwa na watu kama Fidel Castro, alikuwa anakutana na watu weusi waliokuwa wageni kwenye mbinu Za kivita, na mara zote hakufanikiwa lakini Walau aliwaachia ujumbe Cuba ambao Pamoja na udogo wao uliwapa imani kubwa Zaidi. Aliwaaga kwa kuwaambia HASTA LA VICTORIA SIEMPRE.  Alimaanisha Kuwa MPAKA TUSHINDE SIKU ZOTE. Nami nachukua nafasi hii kusema kwaheri Steven Gerrard, unaondoka lakini mashabiki na timu yako unayoipenda itabidi waishi moyo wako, itabidi wakukumbuke daima, hukuwahi kufunga kama Ronaldo,  hukuwahi kukaba kama Makelele, hukuwahi kukimbia kama Bale, hukuwahi Kuwa mpiga pasi kama Xavi, lakini uliwahi kufanya nusu ya kila hicho hapo juu kwa wakati mmoja,  uliikabia Liverpool, ukaifungia Liverpool, ukaikimbilia Liverpool, na ukapiga pasi nyingi kwa sababu yao.  Kuna kitu kimoja tu ambacho unaweza kuondoka nacho Liverpool ambacho usingeweza kukipata kwingine, Upendo. Amini Utapendwa daima,  wanaweza wasikulilie tena lakini uchungu wao utakuwa zaidi ya Nguva, hatoi machozi lakini ndie kiumbe anaumia zaidi. Binafsi nitakukumbuka kwa Mengi, wapo watakaokukumbuka kwa Mengi zaidi, lakini unabaki kuwa mchezaji wa kipekee kuishi. Ule moyo wako wa kuambiwa utapewa Ngog na kugombea naye ubingwa, nafasi ya Suarez atarithi Balloteli, kwa Alonso atasajiriwa Aquialani aliye majeruhi ndo wa ajabu zaidi. Siwezi kuita ujinga lakini imani yako ni ya kipekee. KWAHERI STEVEN GERRARD CAPTAIN FANTASTIC,  HASTA LA VICTORIA SIEMPRE. Waache vijana wafanye kazi, bahati mbaya kwa sasa wanaliliwa akina Raheem Sterling, ila acha tuendelee kuamini Kuwa utaacha moyo kama alouacha Che Guevara pale Cuba,  ule wa Mpaka ushindi siku zote.

Ahsanteni By Nicasius Coutinho Suso

0 comments:

Post a Comment