Facebook

Saturday 22 November 2014

Mchezaji mwingine kutoka Brazil awasili Yanga akipishana na Jaja.

Kiungo mkabaji raia wa Brazil Emerson De
Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku
ya jumanne mchana jijini Dar es salaam kwa
ajili ya majaribio katika klabu ya Young
Africans na endapo atafuzu moja kwa moja
atajiunga na mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu
Tanzania bara.

Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye
kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC
iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil,
msimu uliopita alikuwa akicheza soka la
kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow
Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini
humo.

Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini
unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa
kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos "Jaja"
kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda
kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza
kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na
matatizo ya kifamilia.

Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika
kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye
Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika
huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo
yamepelekea kushindwa kurejea nchini
kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao
kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.

Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young
Africans kubakia na wachezaji wanne tu wa
kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna
Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho
hivyo endapo Emerson atafuzu atakua
anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa
kimataifa
Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na
vipimo atajiunga na kikosi cha kocha mbrazil
Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji
ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea
kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom
pamoja na mashindano ya kimataifa.

Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa
mapumzikoni kwa takribani wiki mbili,
kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu
katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola
kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe
pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania bara.

0 comments:

Post a Comment