Facebook

Monday 24 November 2014

MUELEKEO WA LIVERPOOL: BRENDAN RODGERS ALIPOTUNGA MTIHANI WENYEWE WASAHIHISHAJI WENGINE

You'll Never Walk Alone, moja ya nyimbo
maarufu kabisa katika viwanja vya soka. Nyimbo
ambayo pengine inaimbwa na vilabu zaidi ya vitatu
duniani lakini hapana shaka ikisikika tu watu
hutambua Liverpool wapo uwanjani. Ni nyimbo
ambayo maneno yake hukupa imani ya kuvuka mto
kwa miguu.

Hii uwaleta walevi na wale wasio mahala
pamoja, wakorofi na wastaarabu sehemu moja na
washika dini kwa wapagani sehemu moja. Ikiimbwa
hii kila mmoja uelewa jambo moja tu, Liverpool. Ni
nyimbo hii ambayo Simao Sabrosa alibaki akishangaa
na asiamini kama timu aloifunga ilikuwa
inashangiliwa kuliko yake iliyoshinda, ni sababu hii
ambayo Thiery Henry aliwahi kukiri Anfield ni
sehemu ambayo yeye hupenda kucheza.

Naamini
hata Gerrard ni nyimbo hii ndio inampa sababu
kadhaa za kuendelea kuwa pale. Lakini Kuna tofauti
moja kubwa katika hii nyimbo nayo ni wakati. Wakati
umepita sasa na nyimbo inaimbwa vile vile lakini
katika maadhi tofauti. Namna mbili tofauti, wakati
kipindi Mike Tyson akiwa ananyanyasa ulingoni na
Liverpool ilikuwa moja ya timu ambazo usingejiuliza
Mara mbili katika timu mbili bora zaidi Uingereza,
wakiwa na ugonjwa wao usiokoma(ukame wa ligi kuu
Uingereza) bado walibaki timu iliyotoa mwanga katika
upande wa pili(makombe mengine). Walau nyimbo ya
YNWA ilikuwa sahihi Sana kutumika, ilitumika kwa
ufasaha.

Kila siku ungewaza Kuna anga la Dhahabu
mbele Yao, walikuwa na upande wa kujipigia kifua
kule Ligi ya mabingwa Ulaya. Umeiona Liverpool ya
sasa? Umeitizama inavyocheza? Unamjua mchezaji
wao bora mpaka sasa? Mechi bora walioicheza
mpaka Leo ni mechi ya kirafiki dhidi ya Borrusia
Dortmund. Kama Kuna msimu ambao ile nyimbo Yao
ilitendewa haki basi ni msimu ulioisha, na kama Kuna
msimu ambao ile nyimbo ilitakiwa kuimbwa kwa
nguvu zaidi basi ni msimu huu. Kuna wakati
inakupasa kujiuliza, tatizo ni nini. Je ni wachezaji
wapya? Je ni Suarez kuondoka? Ama ni Sturridge?
Wengi watasema Suarez lakini Liverpool walijua fika
huyu bwana angeondoka, inaweza kuwa shida Sana
lakini bado napata wasiwasi.

Ukiitazama Liverpool ya
sasa unapata zaidi ya maswali 10 kwa wakati mmoja.
Lakini maswali yote kwa wale wasiopenda shida
anaweza kukujibu kwa namna moja tu, MTIZAME
KOCHA. Hata Mimi nimewaza hivyo pia acha
nimtizame Brendan Rodgers. Najaribu kujiuliza je ni
huyuhuyu aloitengeneza Liverpool iliyokuwa
inamaliza michezo yake katika kipindi cha kwanza?
Ni huyu alokosa ubingwa kutokana na kuteleza kwa
kipenzi cha washabikibwa Liverpool? Kwa kuwa
yupo mbali ikabidi nitizame mwenendo wake ili nijipe
Majibu sahihi mwenyewe. Kama Kuna meneja
ambaye aliingia msimu mpya akiwa na Imani kubwa
basi hapana shaka jina la Brendan Rodgers litakuwa
miongoni mwa wale waliokuwa wanaongoza hiyo
orodha.

Huitaji akili nyingi kujua hili. Brendan aliamini
ametengeneza filosofia ambayo iliwatesa na
ingeendelea kuwatesa wapinzani. Ni filosofia ambayo
wachache ufanikiwa nayo haswa kama Una mchezaji
mwenye jina kubwa klabuni. Brendan Rodgers
aliamini ametengeneza "free flowing team" yaani
timu yenye mtirirko huru na ndio maana si ajabu
kuona kuwa alikuwa na washambuliaji waliofunga
magoli mengi zaidi na akawa na beki aliyefunga goli
nyingi zaidi. Kwake jukumu la mchezaji la awali
lilikuwa ushambuliaji na sio uzuiaji na ndio maana Sio
ajabu kuona mchezaji aliyekuwa anatumika kama
kiungo wa Ulinzi kuongoza orodha ya waliosaidia
upatikanaji wa magoli mengi katika ligi. Hapa Rodgers
aliamini kaweza, hata Mimi niliamini hivyo, hapana
shaka hata wewe msomaji pia. Ungempinga vipi
wakati ameshakuonyesha uwanjani? Kama Kuna vitu
Liverpool walishavijua vinakuja basi ni suala la Luis
Suarez kuondoka.

Hapa ndipo hesabu za Rodgers
katika wepesi zaidi zilipoanzia. Katika kalamu na
karatasi yake alijiuliza kilichowanyima ubingwa
msimu uliopita, Jibu akapata jepesi kabisa na haraka,
ilikuwa safu yake ya ulinzi. Kisha akatizama timu
yake ilifunga magoli mangapi akagundua kuwa kama
angeondoa magoli ya Suarez Liverpool bado ilikuwa
inasalia kuwa timu ya pili nyuma ya Man City kwa
magoli mengi. Hapa ndipo maamuzi yake SAHIHI
yalipokuja. Mtu wa muhimu kabisa wa kuziba pengo
la Suarez alitakiwa kwanza atoke katika safu ya
Ulinzi, Kisha alihitaji mtu wa ushambuliaji ambaye
angeweza kumpatia magoli walau 16/18 maana yake
anagalu nusu ya alofunga Suarez. Hapa ndipo
mawazo ya aina ya kina Falcao yakapotea, aliamini
aina hii ingetaka itizamwe yenyewe kabla ya timu
jambo ambalo lingeharibu utaratibu. Na katika ulinzi
apunguze magoli ya kufungwa walau kwa nusu
yabaki 25 kutoka 50. Hapa Liverpool ingefunga
magoli machache kuliko msimu uliopita lakini
wangekuwa na wastani mzuri wa tofauti ya magoli ya
kufunga na kufungwa kuliko msimu uliopita. Hapa
ndipo Rodgers alipofungia mahesabu na kuamini
kuwa ameandaa mtihani mpya ambao wapinzani
ungewatoa jasho.

Pamoja na kwamba wasahishaji
wangekuwa hao hao ila kuyajua Majibu yake
ingekuwa ngumu Sana. Hapa akafungua pochi
akaelekeza nguvu katika maeneo yenye shida zaidi,
ulinzi na kiungo basi akaitafuta fukwe ya Miami ilipo
huki taratibu akisubiri kuamua Kati ya Balloteli na
Remy nani aingie. Bahati mbaya alisahau vitu 3 vya
msingi. Tatizo kubwa la ulinzi lilikuwa kiungo mkabaji
wa asili( Heshima kwa Gerrard ndio dhambi pengine
inayomtafuna), Kiwango na matumizi ya Henderson
(huyu ndio alikuwa nguzo ya Liverpool) pia
hakukumbuka Afya ya Sturridge. Hapa ndipo mtihani
wake ulipovuja, hapa ndipo kila meneja amepata
Majibu, bahati mbaya hakuna muda wa kutunga
mwingine, na hii ndio adhabu ya kalamu yake
mwenyewe. Unamfahamu Napoleon Bonaparte moja
ya viongozi wenye roho ngumu na ya kigaidi kuwahi
kuiongoza Ufaransa. Aliwahi kusema " Dini ndio
sababu inayowafanya masikini wasiue matajiri" hapa
ndipo mashabiki wa Liverpool walipo. Wanaishi katika
dini yenye imani kali, wameishi wakiamini Kuwa
Huwezi Kutembea Peke Yako, ukiharibu tumeharibu
wote.

Nyimbo ya YNWA ni msingi mkubwa
unaowaongoza, bahati mbaya mdomo unaimba lakini
rohoni wengi wanatamani kumuazima Roman
Abramovich utendaji. Usahihi wa hii nyimbo sio
wakati huu, sio wakati ambao Liverpool inafungwa
mechi tano mfululizo. Usahihi wake ni kama msimu
uliopita unaimba ukiamini ukifungwa Leo utafurahi
katika mechi 7 au 8 zijazo. Hata Bob Peasley na Bill
Shankly makocha waliotengenezewa sanamu katika
malango ya uwanja waliweka utaratibu huu. Brendan
Rodgers anaishi katika kivuli hiki, dini hii ina utaratibu
unaomlinda. Utaanzaje kwenda na bango la Brendan
Out wakati kabla na baada ya mechi unaimba You'll
Never Walk Alone.( hutokaa utembee mwenyewe).
Lakini kila nikitizama mwenendo wa Liverpool sidhani
kama yupo salama Sana. Wale wamiliki akina Henry
ndio watu pekee ambao hawaishi katika hii dini, wao
wanaamini katika michezo mingine kabisa.
Ningekuwa na uwezo ningemtumia Brendan ujumbe
mfupi tu, "UNAIJUA DINI YA HENRY. Najua jambo la
kwanza angekumbuka King Kenny Dalglish.

Muda
unaenda na usalama wa Brendan upo katika mikono
miwili tu. Ya kwake mwenyewe na ya wapinzani. Hata
hivyo mwandishi maarufu Maggie Ghallager aliwahi
kusema hakuna kazi ngumu kama ya kuwa mwalimu
mzuri. Hata Nyerere hakufanikiwa hapa ndio maana
wapo wanaompinga hadharani. Hata Brendan yupo
hapa ndio maana naweza kuyatabiri maamuzi ya
John Henry, naamini hata wewe ushayajua. Tatizo la
Brendan ni moja tu mpaka sasa mtihani alotunga
ulivujia kwa wasahihishaji wengine. Sioni Liverpool
ikibadilika karibuni kabla ya kocha hajabadilika.

0 comments:

Post a Comment