Facebook

Friday, 16 May 2014

Wizara ya Maliasili Inaongozwa kwa Ubabaishaji


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Wizara ya Maliasili na Utalii inaongozwa kwa ubabaishaji na ‘mvutano wa kimasilahi’ baina ya waziri na katibu mkuu, hivyo kukwamisha shughuli za kuendeleza utalii.

Msemaji wa kambi hiyo (Maliasili na Utalii), Mchungaji Peter Msigwa alitoa kauli hiyo juzi wakati akisoma maoni kuhusu hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka 2014/15.


Alisema kambi ya upinzani inasikitishwa na mvutano baina ya Waziri Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wake, Maimuna Tarishi ambao unaonyesha udhaifu wa Serikali.


“Hii inathibitisha kuwa Serikali ni dhaifu kwa kuwa, waziri na katibu mkuu wa wizara moja wanafanya kazi bila kushirikiana na kila mmoja anaonekana kumvizia mwenzake hadharani badala ya kukaa kwa pamoja kutekeleza maazimio ya Bunge,” alisema Msigwa.


Alisema kitendo cha Waziri Nyalandu kuwasimamisha kazi wakurugenzi wawili, lakini wakarudishwa na katibu mkuu huku akisema taratibu za kuwafukuza hazikufuatwa na hii ni dalili kuwa hata yeye (Nyalandu) siyo msafi kwa kuwa anashindwa hata kujua mipaka yake ya kazi.


Mbali na mvutano huo, Msigwa alisema maazimio ya Bunge kuhusu matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili yanaendelea kupuuzwa na watumishi wenye tuhuma wakihamishwa vitengo.


“Ngoma ikivuma sana hupasuka, tena Mungu siku zote hamfichi mnafiki na debe tupu haliachi kutika (siyo maneno yangu, bali ya wahenga). Siyo mara ya kwanza kambi ya upinzani kuhoji juu ya usafi wa Lazaro Nyalandu,” alisema.

0 comments:

Post a Comment