Facebook

Tuesday 27 May 2014

Papa awashutumu mapadri wanaolawiti maKanisani



Papa Francis akiomba karibu na ukuta unaotenganisha Bethlehem na Jerusalem.
Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, amewasili Roma baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu Mashariki ya Kati ambapo alisema kuwa tabia ya baadhi ya mapadri Wakatoliki waliokuwa wakiwanyanyasa watoto wadogo kingono kanisani inaweza kulinganishwa tu na misa ya Mashetani.
Baba Mtakatifu alifanya ziara ambayo ilihudhuriwa na maelfu ya watu wa imani tofauti katika eneo hilo na wachambuzi wengi wamesema kuwa imekuwa ya kufana.
Wengi wanasema kuwa Baba Mtakatifu kulinganisha vitendo vibaya vya ngono walivyofanyiwa watoto na mapadri na misa ya mashetani ni lugha nzito hasa ikitambuliwa kuwa tayari Papa Francis amewahi kuomba msamaha kwa vitendo hivyo kote duniani.
Vitendo hivyo vimeharibia sifa Kanisa Katoliki kwa muda mrefu sasa.
Taarifa kutoka makao makuu ya Papa yanasema kuwa kwa mara ya kwanza tangu yeye achukue wadhifa wake anatarajiwa kukutana na wale walionyanyaswa na mapadri kingono.
Wakatoliki wengi walikasirishwa na vitendo hivyo na wamefurahi kuwa Papa anaweza kuomba msamaha na kisha akutane na walioathirika na wengi wanasubiri kusikia atakachowambia atakapokutana nao.
Hata hivyo iwapo Papa anataka kuaminiwa zaidi itabidi awaadhibu wanaume waliofanya vitendo hivyo na wale Kanisani waliokuwa wakiwaficha waliofanya makosa hayo wanapaswa kuachishwa kazi Kanisani.
Papa anaweza kujivunia ziara yake Mashariki ya Kati kwa kuwa alipoanza alisema ziara yake ingekuwa ya Dini na wala sio siasa. Ni dhahiri kuwa katika Mashariki ya Kati ni vigumu kufahamu kule siasa zinakoanzia na Dimi kumalizika.
Kwa mfano uamuzi wa Papa kusimama kando ya Ukuta uliojengwa na Israil kutenganisha Bethlehemu na Jerusalem kumemwingiza katika siasa kwa sababu ukuta huo ni ishara kamili ya utengano na siasa zinazotenganisha Wayahudi na Wapalestina.
Ni wazi kuwa wakati huu Papa anafahamu mengi kuhusu siasa za Mashariki ya Kati kama anavyofahamu maswala ya Dini.

0 comments:

Post a Comment