Na Dustan Shekidele, Morogoro
AMA kweli dunia ina mambo na mambo yenyewe ndiyo haya! Katika hali ya
kushangaza, mwanaume aliyefahamika kwa jina la Ramadhan Ally, mkazi wa
Kata ya Mbuyuni Manispaa ya Morogoro amewashangaza wengi kufuatia uamuzi
wake wa kukodi ngoma ya asili kwa lengo la kwenda kumfumania mkewe
aliyejulikana kwa jina moja la Asha.
Tukio hilo lililofunga mtaa lilijiri asubuhi ya saa 3:14 Jumatatu
iliyopita eneo maarufu kwa jina la Sultani baada ya mwanaume huyo
kutonywa kuwa, mke wake alikuwa amelala kwa rafiki yake kipenzi,
Abdallah Elias.
Baadhi ya wananchi waliobahatika kuwasili katika eneo la tukio
walishuhudia mwenye mali akiwashushia kichapo kikali ‘wasaliti’ hao
ambapo vurugu zikapamba moto.
Kufuatia hali hiyo, viongozi wa serikali ya mtaa huo waliamua kutoa
taarifa kwa Kamanda Mkuu wa Ulinzi wa Jadi Kata ya Mbuyuni, Aidan Mtimbo
ambaye alifika eneo la tukio na vijana wake na kuwasomba watuhumiwa hao
msobemsobe huku wakisindikizwa na ngoma hiyo hadi Kituo cha Polisi Kata
ya Mbuyuni.
Katika hali ya kushangza, nje ya kituo hicho cha polisi baadhi ya
wananchi waliokuwa na hasira walishinikiza watuhumiwa watolewe nje
wawafanyie kitumbaya huku baadhi yao wakikipopoa mawe kituo hicho
kilichokuwa na askari mmoja aliyevaa nguo za kiraia.
Baada ya vurugu hizo, afande huyo alipiga simu kituo kikuu cha polisi
kuomba msaada ambapo askari wa pikipiki walifika na kuwakodia teksi
watuhumiwa hadi kituoni.
Mwandishi wetu alifanikiwa kuwahoji wahusika wote watatu ambapo mume wa
mwanamke huyo ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumza kama ifuatavyo:
“Huyu mwanamke ni malaya sana, kwanza nimemtoa kwao Matombo (Morogoro) akiwa na watoto wawili na kila mmoja na baba yake.
“Mimi sikujali hilo, ukipenda bonga penda na ua lake. Miezi mitatu
iliyopita aliniambia ana ujauzito wangu, taarifa hizo zilinifurahisha
sana. Cha ajabu juzi akaniambia ametoa mimba yangu, nilipomuuliza kwa
nini, akasema kwa ujeuri eti hayupo tayari kuzaa na mimi kwa sasa.
“Nilichukua uamuzi wa kumrudisha kwao, jana usiku napokea taarifa kuwa yuko nyumbani kwa rafiki yangu kipenzi, Abdallah Elias.
“Ndiyo asubuhi nikakodi ngoma na kwenda, niliwakuta wamelala kitandani.”
Kwa upande wake Elias alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alisema:
“Huyu mwanamke ni mbaya sana, ametuchanganya mimi na rafiki yangu
Dullah, yeye kaja kwangu jana Jumapili akaniambia amefukuzwa na mumewe
hivyo anaomba alale kwangu kesho yaani leo aende kwao Matombo kumbe
alisharudishwa kwao toka juzi.”
Naye mwanamke huyo alipohojiwa na paparazi wetu alikuwa na haya ya kusema:
“Huyu mwanaume (Ramadhan) hajanioa, kila siku nikimwambia twende kwa
wazazi wangu ananipiga danadana. Ni kweli nimetoa mimba yake, siko
tayari kuzaa naye mtoto nje ya ndoa. Huyu Elias, yeye alionesha nia ya
kunioa.”
Diwani wa Kata ya Mbuyuni, Samuel Msuya amethibitisha kutokea kwa
fumanizi hilo kwenye mtaa wake lakini aliwatupia lawama polisi wa
pikipiki kwa kupuuza uongozi wa juu wa kata hiyo ambao kwa kushirikiana
na walinzi wa jadi walifanikiwa kuwalinda watuhumiwa wao na kufika
salama kwenye kituo cha polisi.
0 comments:
Post a Comment