Polisi walifika eneo la tukio majira ya saa saba mchana ikiwa ni saa 18 tangu kutokea kwa ajali hiyo ambapo baada ya kumaliza kazi ya kukagua na kupima eneo la ajali, mwili huo ulihamishiwa chini ya mti kuukinga na jua usiharibike wakati wakisubiri daktari kuja kuufanyia uchunguzi.
Tanzania Daima ilishuhudia wananchi na viongozi wa Kata ya Engaruka wakiulinda mwili huo wakati akisubiriwa daktari kutoka Mto wa Mbu ambaye naye alifika eneo la tukio majira ya saa 10 jioni.
Ajali hiyo ilitokea Juni 12 mwaka huu baada ya Shamba kudondoka kutoka kwenye gari la mizigo aina ya Toyota DCM, lenye namba za usajili T 995 AMB lililokuwa likitokea mnadani Engaruka kwenda Kijiji cha Selela.
Diwani wa kata hiyo, Pashet Sengerwan (CCM), alisema kuwa mwili huo ulifanyiwa uchunguzi kwenye eneo la ajali kisha kuzikwa Juni 13, majira ya saa 11 jioni kwenye makaburi ya kijijini hapo bila kuwasubiri ndugu zake waliokuwa wakitokea Singida.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema tayari wameshamhoji mmiliki wa gari hilo, Sauli Kitomari huku wakiendelea na juhudi za kumtafuta dereva wa gari hilo ambaye alitoroka mara baada ya kutokea ajali hiyo.
Alisema kuchelewa kwa polisi kufika eneo la tukio, kulitokana na kukosekana kwa kituo cha polisi kwenye eneo la Engaruka ambalo pia lina tatizo la mawasiliano ya simu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moduli, Dowika Kasunga, alisema hali hiyo ilisababishwa na tatizo la mawasiliano na mamlaka husika kwani katika Kata ya Engaruka ili upige simu, lazima uende umbali mrefu kutafuta mawasiliano hayo.
0 comments:
Post a Comment