Ada hizo kwa wale wa ngazi za cheti na stashahada ambazo zimeongezwa kwa karibu mara mbili au zaidi ya zile zilizokuwa zikilipwa awali.
Uamuzi huo ambao huenda ukawaathiri zaidi wanafunzi ambao waliona ualimu kama kimbilio, unaelezwa na baadhi ya wadau wakiwamo walimu, wanafunzi na hata wakufunzi wa baadhi ya vyuo nchini kuwa ni wa ghafla.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakufunzi, uamuzi huo umetolewa kupitia waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na unatarajiwa kuanza kutekelezwa muhula wa pili wa masomo utakaoanza Julai 2, mwaka huu.
Kabla ya kupandishwa kwa ada hizo, wanafunzi wanaosomea ualimu kwa ngazi ya cheti walikuwa wakilipa Sh200,000, lakini sasa watalazimika kulipa Sh300,000, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.
Kwa wale wanaochukua stashahada watalazimika kulipa Sh400,000 kwa masomo ya Sanaa na Sh600,000 kwa masomo ya Sayansi kutoka Sh200, 000 za awali.
Mhasibu wa Chuo cha Ualimu cha Mtwara, aliyekataa kutaja jina lake kwa kuwa siyo msemaji wa chuo hicho, alithibitisha kupokea waraka wa Serikali unaowataka kupandisha ada, lakini alisisitiza kuwa Mkuu wa Chuo ndiye angeweza kufafanua zaidi kuhusu ongezeko hilo.
“Taarifa hizo ni za kweli ada imepanda, kama umezipata kutoka wizarani hivyo ndivyo ilivyo kwa hiyo huna sababu ya kupata taarifa zaidi kutoka kwetu,” alisema mhasibu huyo.
Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na uhaba wa fedha na ugumu wa kuviendesha vyuo hivyo.
Habari zinasema kwa muda mrefu sasa, Serikali imekuwa ikidaiwa na wazabuni fedha nyingi, jambo ambalo limeathiri pia uendeshaji wa vyuo vikiwamo vya ualimu.
Baadhi ya wakufunzi wameeleza kuwa fedha za ada sehemu yake itatumika kutatua matatizo ya uhaba wa fedha ambao umekuwa ukiwakabili na hivyo kuathiri utoaji wa huduma zikiwamo za vyakula.
Wizara ya Elimu
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema viwango vilivyoongezwa siyo vikubwa ikilinganishwa na hali ya ugumu wa maisha ilivyo sasa nchini.
“Unamweka mtu mwaka mzima anakula, analala, anasoma…kweli unaona hiyo ada hiyo ni kubwa? Bado siyo kubwa kiasi cha kushtua watu,” alisema Bunyazu.
Aidha, Bunyazu alisema kuwa wanafunzi watakaopata daraja la kwanza katika masomo ya Sayansi na Hisabati na kuingia katika vyuo vya ualimu vya Serikali watasomeshwa bure na wale watakaopata daraja la pili na la tatu watapewa mkopo.
Wengine wazungumza
Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventura akizungumzia suala hilo jana, alisema kuwa siyo kweli kwamba serikali haina fedha za kutosha ndiyo maana inaongeza ada, ila inadhani kuwa idadi ya walimu waliopo inatosha.
“Serikali imeamua kupandisha ada kwa kudhani kuwa walimu waliopo wanatosha, lakini ikumbuke kuwa kuna walimu wengi wazee wanaostaafu kila mwaka, wengine hawaripoti shuleni, hivyo tunahitaji kuwa na benki ya walimu,” alisema Boniventura.
0 comments:
Post a Comment