Vitimbi, vituko, na kejeli zilitawala jana makao makuu ya klabu ya Simba wakati wagombea uongozi wakirudisha fomu, huku mgombea urais, Michael Wambura akiambatana na viongozi wa dini waliomwaga sala.
Wambura, ambaye amekuwa akisaka uongozi wa ngazi mbalimbali bila ya mafanikio tangu mwaka 2008, alirudisha fomu akiwa kwenye gari la wazi ambalo lilisukumwa na mashabiki ambao walikuwa wakipiga kelele kusema ‘rais...rais...rais”
Lakini mgombea wa nafasi ya makamu wa rais, Geofrey Nyange, ambaye alijiuzulu nafasi hiyo mwaka jana, akijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kumzomewa.
Siyo hivyo tu, wanachama hao walishika mabango mbalimbali ambayo yalikuwa yanampamba Wambura kuwa ndiye rais anayestaili kuiongoza klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Baadhi ya mabango hayo yalikuwa yanasomeka, “Dalali wewe sio nabii Simba, Aveva ulipata kura mbili DRFA (Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam) Simba taasisi kubwa.”
Wambura aliambatana na mchungaji Godlove Kirivato kutoka Kanisa la Ufufuo wa Uzima, linaloongozwa na Mchungaji Gwajima pia alikuwa Ustadhi Abdurahman Ahmed ambao waliangusha dua ya kumtakiwa heri Wambura ambaye ana historia ya kuenguliwa kwenye chaguzi mbalimbali kwa kigezo cha kuvunja katiba ya Simba na ukosefu wa uadilifu.
Wambura aliitaka Kamati ya Uchaguzi itoe nafasi kwa wanachama wa klabu hiyo kuchagua viongozi wanaowataka.
“Wanachama wasikilize sera. Uongozi ni dhamani hivyo kamati ya uchaguzi nayo iwape nafasi watu wachague viongozi wanaowataka, kwa kuwa kwa miaka mingi Kamati imekuwa ikichagulia wanachama viongozi.” alisema Wambura ambaye aliwahi kuwa katibu wa TFF, Chama cha Kriketi na mwenyekiti wa Simba.
Nyange alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kundi la wanachama kumzonga huku wakiimba Julio, Julio, Julio kumaanisha kocha msaidizi wa zamani wa Simba.
Katibu wa Kamati ya Uchaguzi, Khalidi Kamguna aliwataja wagombea waliochukua kuwania urais kuwa ni Evans Aveva, Wambura na Andrew Tupa wakati wanaowania nafasi ya makamu wa rais ni Nyange, Joseph Itang’are, Sued Nkwabi, Bundara Kabulwa, Willbar Mayage na Jamuhuri Kihwelo ‘Julio’.
Wanaowania ujumbe ni Jasmine Badawi, George Wakuganda, Asha Muhaji, Asha Kigundula, Abdulhamid Mshangama, Alfred Martin, Ally Sulu, Iddy Kajuna, George Wakuganda, Said Tuli, Ramson Athuman, Seleiman Abdul, Khamis Mkoma, Said Pamba, Rodney Chiduo.
Wengine ni, Collin Frisch, Chano Almas, Emmanuel Kazimoto, Juma Pinto, Salim Jazaa, Yassin Said, Hussein Simba, Damian Manembe, Ally Chaurembo, Ibrahim Masoud ‘Maestro’, Ahmed Mlanzi, Iddi Nassoro, Kessy Kikoti, Maulid Said, Juma Mussa, Omary Said na Said Kubenea.
0 comments:
Post a Comment