Siyo
rahisi kwa mtu ambaye anapata chakula kutwa mara tatu, kuamini kuwa kuna
binadamu ambao wanaweza kuishi hata siku tatu bila kupata hata mlo
mmoja.
Hata
hivyo ni ukweli usiopingika kuwa wakati unakula na kumwaga chakula
kwenye mifuko ya takataka, wapo ambao hutamani kukimbilia mifuko hiyo na
kujitafutia chochote kwa ajili ya matumbo yao.
Wapo
ambao hudiriki kula hata vitu ambavyo havistahili kuliwa na binadamu,
lakini hawana jinsi wanafanya hivyo kutuliza matumbo yao yanayosumbuliwa
na njaa.
Njaa
imekuwa ni tatizo sugu linaloonekana kujitokeza katika mataifa
mbalimbali yanayoendelea, huku bara la Afrika likiwa limeathirika kwa
sehemu kubwa kutokana na janga hili.
Licha ya
kuwa na eneo kubwa la ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha, ukanda wa
Afrika Mashariki nao umekuwa ukikumbwa na baa hili katika baadhi ya
maeneo.
Hilo
linatokana na maeneo hayo kuwa na ukame na kukosa mvua, hali
inayopelekea kilimo kutofanyika kama inavyostahili hivyo chakula kuwa
miongoni mwa vitu hadimu kupatika kwa wakazi wa eneo husika.
Kijiji
cha Kakoghit kilichopo kwenye Kata ya Lokis nchini Kenya, kimekuwa
miongoni mwa maeneo ambayo yapo katika hali mbaya zaidi kutokana na
tatizo la njaa.
Tukio la
hivi karibu la familia moja kuchinja paka na kumla kama kitoweo baada ya
kuzidiwa na njaa waliyokaa nayo kwa siku kadhaa kutokana na kukosa
chakula, limedhihirisha namna gani njaa ilivyokuwa tishio.
Familia
hiyo yenye jumla ya watu watatu ikiwajumuisha Jepoterit Yaranyang (80),
Jepteker Ng’uriawing (35) na mtoto wake wa miaka miwili ilifikia uamuzi
wa kumuiba paka wa jirani na kumchinja ili kutuliza njaa iliyokuwa
ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Katika
mahojiano yake na gazeti la moja nchini Kenya, Ng’uriawing anasema kuwa
baada ya kukaa siku nyingi bila kula huku mama yake akiwa hoi kitandani
akidhoofika kutokana na njaa, akafikiria kumkamata paka wa jirani ili
wamfanye kitoweo. Wazo hilo likatawala kichwani mwake na dakika chache
alipokatiza paka huyo alimpiga kichwani kabla ya kumchinja na kuchoma
nyama yake kuitafuna ili kupoza njaa iliyokuwa ikiwakabili.
“Baada ya
kuona hali inazidi kuwa mbaya nikaona tutaangamia kwa kuwa mama yangu
tayari alishaanza kudhoofika kutoka na njaa, nikaamua kumgonga paka
kisha nikamchuna ngozi na kuchoma nyama yake ambayo ilikuwa na damu
nyingi”anasema Ng’uriawing na kuongeza:
“Ukweli
ni kwamba hali ilikuwa mbaya sana hata kama paka asingejitokeza
ingewezekana ningemchinja mtoto wangu tuile nyama yake maana nisingeweza
kuvumilia hali ya njaa kali kiasi kile”.Mmiliki
wa paka huyo, Chepochegheh Todong’ira alimtafuta paka wake mpaka
kufikia hatua ya kukata tamaa lakini alipozunguka kwenye nyumba ya
jirani yake alikuta mabaki ya mifupa, ngozi na mkia.
Anasema
alipojaribu kuhoji familia hiyo walimweleza wazi kuwa walimchinja paka
huyo na kumfanya kitoweo kutokana na kukabiliwa na njaa kali.
Baada ya
kupewa majibu hayo yaliyomtia simanzi Todong’ira alitoa taarifa kwa
chifu wa eneo hilo na kumfahamisha namna ambavyo hali ilivyo tete mpaka
kufikia hatua ya binadamu kuchinja paka.
“Nilipomuhoji
Jepteker hakukanusha alikubali kuwa wamemchinja paka wangu kutokana na
njaa, kiukweli hali ni mbaya sana huku kwetu na Serikali imetusahau
kabisa inapaswa kuleta chakula katika eneo hili,” anaeleza.
Wakati
mahojiano yakiendelea kikongwe Yaranyang alikuwa hoi kitandani huku
akionekana muda wowote anaweza kukata roho kutokana na kukosa chakula.
Naibu
Chifu wa Kata ya Lokis, Johnston Long’iro alifika katika nyumba hiyo na
kukuta mabaki ya paka huyo na kujihakikishia kwa kiasi gani hali ni
mbaya.
“Hali ya
njaa ni mbaya sana hapa kwetu watu wengi wamefikia hatua ya kuhamia
katika maeneo jirani kama Elgeyo-Marakwet na Pokot Magharibi ambako
wamekwenda kutafuta chakula na lishe na maji kwa mifugo yao,” anasema
Long’iro.
Anaongeza
kuwa njaa pia imeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu katika eneo
hilo, huku shule za msingi kadhaa zikiwamo Korelech, Krezeek na Ng’aina
zikiwa hazijafunguliwa kutokana na wanafunzi na wazazi wao kuhamahama
wakitafuta chakula.
Anafafanua
kuwa mara ya mwisho chakula cha msaada kupelekwa katika eneo hilo ni
mwaka uliopita na shughuli hiyo ilioongozwa na Shirika la Chakula
Duniani (WFP).
Kisa hiki
kinaweza kuwa mfano mmojawapo wa maisha ya baadhi ya maeneo barani
Afrika, ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na njaa.
Wapo ambao hulazimika kula matunda na mizizi bila kufahamu huenda ikawa na sumu hatua inayowafanya wengine kupoteza maisha.
Endelea kutembelea katemimethsela.blogspot.com uweze kufahamu matukio mbalimbali yanayotokea duniani ambayo huwezi kuyajua kupitia sehemu nyingine
0 comments:
Post a Comment