Dawa za kulainisha nywele (relaxer) zimekuwa zinapendwa na wanawake
wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya
apendeze na awe wa kuvutia.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha
uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo ambazo huingia
mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.
Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata alifanya utafiti na
kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha
uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye
kizazi uitwao fibroids au leimyoma.
“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu
tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya estrogen
ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa fibroids,” anasema.
Dk Chipata anasema kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi
ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.
Utafiti wa Dk Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada
tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa
wa tatizo hili ulibainika.
“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvinbe kwenye kizazi,
zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na za kwenye mafuta ya ngozi kama
vile mercury na hydroquionone,” anasema.
Dk Chipata anasema madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni
makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha saratani au
kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya zebaki (mercury).
“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu
kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi
kutokana na mfumo wa ngozi,” anasema.
Anashauri kuwa ni vyema watu wakasoma kipodozi kimetengenezwa kwa nini
kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au
nywele halisi badala ya kujibadilisha.
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali
kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinyl chloride, zirconium na
bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.
Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dk Lauren Wise na wenzake
nchini Marekani na kuchapishwa kwenye jarida la afya la nchini Marekani
ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen
ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha
mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au
vivimbe hivi hujulikana kama fibroids au myoma.
Tumehamia
katika site hii mpya na bado tuko katika maboresho,hii ni katika hatua za awali
kabisa kuiboresha site yetu na utoaji wa habari na burudani.Vitu vingi
vitaonekana katika site hii mpya hivi karibuni.Endelea kutembelea www.bantutz.com
0 comments:
Post a Comment