Dar es Salaam. Serikali imepoteza zaidi ya Sh362.9 bilioni kutokana na
baadhi ya kashfa kubwa za ufisadi na operesheni mbalimbali
zilizoligharimu taifa tangu uhuru.
Uchunguzi wa mtandao huu umebaini taifa kukumbwa na kashfa mbalimbali za
upotevu wa fedha au kuanzisha mipango ambayo utekelezaji wake
ulisababisha maumivu kwa wananchi na hakuna awamu ya uongozi wa Serikali
iliyokwepa hali hiyo.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeiongoza nchi toka
mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi
(1986-1995), Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete
(2005-hadi sasa), kumeibuka kashfa mbalimbali, saba zikiwa kubwa na
kulitikisa taifa.
Kashfa na operesheni saba kubwa zilizotikisa taifa ni pamoja na
Operesheni Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji
Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS) na Kashfa ya
Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya Richmond, Operesheni
Tokomeza Ujangili na ile ya uchotaji mabilioni katika akaunti ya Escrow.
Operesheni Uhujumu Uchumi
Mwaka 1984 Serikali ilianzisha Operesheni Uhujumu Uchumi, iliyoongozwa
na Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine ili kutaifisha mali ambazo
baadhi ya watu walidaiwa kujipatia kwa njia isiyo halali.
Operesheni hiyo ilishuhudia baadhi ya watuhumiwa wakimwaga fedha mitaani
na majalalani, huku wengine wakitupa mali kuhofia kutiwa kwenye mkono
wa sheria.
Hata hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya watendaji wa Serikali ambao
hawakuwa waaminifu, waliitumia nafasi hiyo vibaya kutaifisha mali za
baadhi ya watu, ambao hawakuwa wahujumu uchumi.
Zoezi hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa vijijini kuwekwa ndani na
wengine kuachwa maskini baada ya kunyang’anywa mali zao ikiwamo mifugo
na mashine za kusaga nafaka, kwa kudaiwa kuwa walizipata kwa njia isiyo
halali.
Mfuko wa Commodity Import Support (CIS)
Miaka 24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka sakata jingine lililokuwa
na harufu kubwa ya ufisadi wa mabilioni katika Mfuko wa Kuwezesha
Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support – CIS).
Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara maarufu
nchini na wizara kadhaa za Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ).
Kupitia mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi ya Sh200 bilioni kwa kivuli cha uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mfuko huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya 1980, ambapo baadhi ya
nchi wafadhili ikiwamo Japan, zililenga kuipatia Tanzania fedha za
kigeni za kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa barabara, vifaa vya
kilimo, ujenzi na vingine mbalimbali. Mpango huo ulioanzishwa na
Serikali uliendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000, ambapo nchi hizo
wahisani ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Norway,
Uswisi, Ubelgiji, Sweden na Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali fedha
za kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.
Wizara zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa CIS ni pamoja na iliyokuwa
ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kazi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya
Maji na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Tanzania Bara, wakati Zanzibar
zinatajwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maji.
Rada
Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine.
Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa
rada kuukuu kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada
hiyo unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa Sh29.5
bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.
Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha hizo kama chenji, huku
ikisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika na ununuzi
wa rada hiyo mtumba, washitakiwe Tanzania au Uingereza kutokana na
kubainika dosari kwenye ununuzi huo.
Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, mtandao
wa Wikileaks unaosifika kwa kufichua siri za ndani ya mataifa mbalimbali
duniani, ulibaini kuwepo kwa harakati nchini za kutowafikisha
mahakamani wahusika wa ufisadi huo.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti
ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ambapo vigogo
kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni katika
akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya
siasa katika kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki wa nyaraka hizo.
Richmond
waka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kulitokea tatizo kubwa la uhaba wa umeme.
Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo.
Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alikuwa mstari wa mbele katika
mikakati hiyo ndipo Kampuni ya Richmond Development (LLC) ilipewa zabuni
ya kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme
nchini Tanesco.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa
kuzalisha umeme kama ilivyodhaniwa, badala yake kulikuwa na michezo
michafu iliyofanyika kwa masilahi ya wafanyabiashara na baadhi ya
viongozi wa Serikali.
Mwaka 2007, sakata hilo lilifika bungeni na aliyekuwa Spika wakati huo,
Samuel Sitta aliunda kamati iliyokuwa chini ya mbunge wa Kyela, Dk
Harrison Mwakyembe ili kuchunguza suala hilo.
Kamati hiyo ilichunguza sakata hilo na kutoa taarifa ilionyesha kuhusika
kwa viongozi wa juu wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward
Lowassa na kusababisha kiongozi huyo, kujiuzulu pamoja na mawaziri
wawili kung’oka madarakani.
Waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, ambao ni Naziri Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Operesheni Tokomeza Ujangili
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na Serikali kupambana na
ujangili wa wanyama nchini mwaka jana iliwang’oa madarakani mawaziri
wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji
wa operesheni hiyo.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya
kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa
shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Khamisi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi
Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo.
Operesheni hiyo inadaiwa kukiuka haki za binadamu ikiwamo watu 13 na
askari sita kuuawa, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa, ubakaji, rushwa na
uporaji wa mali za wananchi.
Akaunti ya Esrow
Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika, mapema mwaka huu imeibuka
kashfa ya upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Esrow katika
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kashfa hiyo inayolitikisa Bunge na Serikali sasa, imetajwa kuwa ni
mwendelezo wa jinamizi la kashfa ikiwa ya saba kubwa kulikumba taifa
hadi sasa.
Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni, ilifunguliwa wakati
kukiwa kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa zamani wa IPTL (VIP
Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa upande
mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande mwingine.
Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa kuchukua kitu chochote hadi pale
mgogoro utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita hicho cha fedha kilichotwa.
Wazungumza
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema
matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na Serikali kushindwa
kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu wanapatikana na makosa
hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kila mara wizi wa fedha za umma unapotokea, Serikali hupata
kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya watu wengi kuamini
kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza azma zao.
“Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani, kuna kulindana sana,
lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi pengine ufisadi usingekuwa
wa kiwango cha juu namna hii,” alisema.
Mhadhiri
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) Faraji Christoms,
alishauri wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa wanatakiwa
kujitathmini upya.
Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa tathmini kuwa ni uzalendo kwa
taifa, elimu kwa maana ya uelewa wa mambo ya kisheria, lugha za
kimataifa na umakini wakati wa majadiliano ya kimataifa na wanaposoma
mikataba ya aina hiyo.
Tuko katika
maboresho hivi karibuni blog hii itakuwa ni site ambayo itaitwa www.bantutz.com ni katika hatua za kuboresha huduma
zetu za kutoa habari,tutakuja katika muonekano mpya na bora zaidi.
0 comments:
Post a Comment