Tatizo! Huku macho ya waigizaji na wadau wake hayajakauka machozi
kufuatia vifo vya ghafla vya mwongoza sinema, Adam Philip Kuambiana (38)
na mwigizaji Sheila Leo Haule ‘Recho’ (26), tasnia imempoteza mwingine,
mwigizaji, prodyuza na mwongozaji filamu mahiri, George Otieno ‘Tyson’
(41).
Kufuatia kifo hicho ambacho pia ni cha ghafla, wadau mbalimbali wa
filamu, wakiwemo wasanii wenyewe wamesimamia mawazo yao kwamba lazima
kuna kitu!
Tyson alifariki dunia Ijumaa usiku akiwa njiani kukumbizwa Hospitali ya
Mkoa ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kufuatia ajali mbaya ya gari iliyotokea
maeneo ya Gairo, Morogoro.
Katika ajali hiyo, mbali na marehemu walikuwemo watu wengine watatu
ambao ni dereva, MC Gladness Chiduo ‘Zipompa’ na mwingine aliyejulikana
kwa jina moja la Nick ambao walijeruhiwa vibaya na kupatiwa matibabu ya
haraka.
WALIKUWA WAKITOKEA WAPI?
Gari walilopata nalo ajali ni Toyota Noah ambalo liliharibika mno. Wote
walikuwa wakitokea Dodoma ambako Ijumaa mchana walirekodi kipindi na pia
kutoa misaada ya madawati 60 kwenye Shule ya Msingi ya Chalula iliyopo
Chamwino kupitia Kipindi cha Mboni Show kinachoongozwa na Mboni Masimba
kupitia Runinga ya EATV.
Mboni yeye kama bosi wa msafara huo alikuwa kwenye gari jingine na watu kadhaa.
KISA CHA AJALI
Kwa mujibu wa chanzo, ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la nyuma la
kulia kupasuka ghafla kisha kufuatiwa na la mbele kushoto hali
iliyosababisha gari hilo kupinduka na kubiringita mara tatu.
“Kwanza ilipobiringita mara moja, Tyson alichomoka kwenye gari,
likabiringita tena mara mbili. Marehemu alipasuka sehemu ya kati ya paji
la uso,” kilisema chanzo na kuanza kulia.
MANENO YA MWISHO YA MAREHEMU
Chanzo kilizidi kusema kuwa wakati marehemu anazingirwa na roho wa mauti
alikuwa akisema ‘najua nakufa lakini nasikitika kuwaacha wanangu.’
KUNA KITU
Kwa upande wa wasanii kutoka tasnia ya filamu Bongo waliozungumza na mtandao huu juzi, walikazia dhana ya kuwepo kwa kitu kinachoondoa uhai
wa wasanii kwa njia ya kufumba na kufumbua.
“Haiwezekani kila kukicha sisi tu. Tena ghafla. Aisee lazima kuna kitu
japokuwa hatujakijua ni kitu gani,” alisema msanii na kiongozi wa Kundi
la Jakaya Theatre, David Mponji ‘Lazi’.
Akaongeza: “Lakini nataka kukwambia kwamba huu ni mpango wa Mungu kabisa
ili tufanye ibada. Unajua asilimia themanini ya wasanii hawaendagi
kanisani wala misikitini? Hapa sasa tunakumbushwa.”
JACOB STEVEN ‘JB’:
“Hii ni too much! Kweli kifo sasa hata mimi nakiona kiko karibu. Nadhani kuna kitu.”
WILLIAM MTITU:
“Da! Sijui mimi niseme nini. Nadhani iko sababu ya kujiangalia, inakuwa kama kuna kitu vile.”
JACQUELINE WOLPER:
“Siamini aisee! Yaani juzi tu Kuambiana, akaja Recho, leo Tyson! Mh!
Pana kitu hapa. Afadhali tungekuwa tumelia mpaka tumekauka machozi.”
WACHUNGAJI, SHEHE WAMSHUKIA MTABIRI
“Ukisema tabiri maana yake umba jambo. Ndiyo maana hata kwenye maandiko
Mungu alimwambia nabii mmoja atabiri mafuvu kuwa binadamu, ikawa hivyo.
“Sasa huyu mtabiri (hakumtaja jina) ambaye amekuwa akisema wasanii
watakufa kwa wingi ndiye ‘mchawi’ wao maana anaumba vifo kwa wasanii,”
alisema Mchungaji Daniel Rashid wa Kanisa la EAGT Tegeta jijini Dar.
Baadhi ya wachungaji waliozungumza na Ijumaa Wikienda nao walionesha msimamo huo kwamba kutabiri ni kuumba.
Naye shehe aliyejitambulisha kwa jina la Hussein alipozungumza na gazeti
hili juzi alisema yeye anaamini mtabiri ambaye amekuwa akisema wasanii
watakufa ndiye mchawi wao.
“Kwanza kwa nini uwatabirie wenzako tu? Kuna nini hapo? Mbona sijawahi
kusikia amejitabiria mwenyewe?” alihoji Shehe Hussein ambaye hakupenda
kuuanika msikiti anaofanyia utumishi wake.
WOSIA MZITO KWA MASTAA
Katika hatua hiyo, viongozi hao wa dini walitoa wosia kwa mastaa
wakisema kwamba katika hali kama hii hakuna njia mbadala zaidi ya
kufanya ibada.
Walisema huenda pia vifo hivyo ni mpango wa Mungu ili kuwakumbusha
kufanya ibada kwani wasanii wanaonekana muda mwingi wapo kazini kuliko
kwenye nyumba za Mungu au hata kumkumbuka kwa maombi tu.
BONGO MUVI: HAKUNA KUREKODI FILAMU
Baadhi ya wasanii wa Bongo Movies waliozungumza na mtandao huu juzi
walisema wanasikitishwa na vifo hivyo kwani kwa sasa imefikia hatua
kwamba wanakosa muda wa kurekodi filamu, muda mwingi wapo kwenye misiba.
“Hatumkufuru Mungu kwani yeye ndiye muumba ila kusema kweli muda mwingi
tunautumia kuzika tu. Filamu za kurekodi zote zimesimama, maana da!”
alisema msanii mmoja akiomba hifadhi ya jina.
MWILI WA TYSON
Mwili wa Tyson ulitarajiwa kufikishwa Dar Jumamosi iliyopita kutoka
Morogoro. Mjadala uliendelea hadi jioni ya juzi kwamba mwili wa marehemu
ukazikiwe wapi kwa vile marehemu ni mwenyeji wa Kenya.
WAZAZI WAKE WAFICHWA
Habari za baadaye zilidai kwamba, hadi juzi jioni taarifa za kifo cha
Tyson zilikuwa zimefichwa kwa wazazi wake kutokana na kile kilichodaiwa
kwamba, hali zao kiafya ni ‘tiamajitiamaji’.
ASILI YA TYSON
Tyson alitua nchini mwanzoni mwa mwaka 2,000 akitokea Kenya. Alipofika
alifanya kazi katika Kituo cha Runinga cha ITV akiwa ni prodyuza wa
Kipindi cha Mambo Hayo.
Hapo ndipo alipomwibua Yvone-Chery Ngatwika ‘Monalisa’ na kumwingiza
kwenye sanaa na baadaye kuwa mchumba wake ambapo mwaka 2001 walifunga
ndoa ya kanisani.
Baadaye marehemu alijitoa ITV na kufanya kazi binafsi huku akiwa
mwongoza sinema mahiri Bongo. Amekuwa mwongozaji wa vipindi mbalimbali
kama Mboni Show cha Mboni Masimba, Wanawake Live cha Joyce Kiria na
vipindi kibao vya TV1.
Tuko katika
maboresho hivi karibuni blog hii itakuwa ni site ambayo itaitwa www.bantutz.com ni katika hatua za kuboresha huduma
zetu za kutoa habari,tutakuja katika muonekano mpya na bora zaidi.
0 comments:
Post a Comment