MTU mmoja aliyedaiwa kuwa ni daktari wa jijini Mwanza, Raymond Simion
(36) amekutwa amekufa ndani ya chumba kwenye nyumba ya kulala wageni
‘gesti’ ijulikanayo kwa jina la Nesta iliyopo Ubungo NHC wilayani
Kinondoni jijini Dar.
Taarifa kutoka katika gesti hiyo zinasema marehemu alijiorodhesha kwenye
kitabu cha wageni kuwa ni daktari wa Hosptali ya Nyamagana jijini
Mwanza na alikuja Dar kikazi kwa muda wa wiki moja. Mauti yalimkuta
akiwa na siku mbili tu tangu alipowasili.
Mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe
gazetini alisema kuwa, daktari huyo alifika katika gesti hiyo Jumapili
ya Mei 4, mwaka huu na kuchukua chumba namba 102.
Alisema Jumatatu ya Mei 5, marehemu aliomba abadilishiwe chumba, akapewa namba 105 ambamo mauti yalimkutia.
Uwazi lilifanikiwa kufika katika eneo la tukio na kufanya mahojiano na
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo NHC, Amani Sizian ambaye
alisema taarifa ya kifo cha daktari huyo aliipokea saa 9: 03 alasiri ya
siku ya tukio ambapo mhudumu wa gesti hiyo ndiye aliyempigia simu
kumjulisha.
Kiongozi huyo aliendelea kusema kuwa mhudumu huyo alimweleza kwamba
marehemu baada ya kuchukua chumba Jumapili alitoka na kurudi saa 3:00
usiku ambapo alilala, lakini kesho yake hakuonekana kutoka.
“Mhudumu aliniambia kuwa baada ya kutomwona asubuhi, hawakumfuatilia
hadi ilipofika saa 9:00 alasiri ambapo walikwenda kumchungulia chumbani
kwake na kumwona katika hali ya kutokuwa hai.
“Ilibidi niende. Nilipofika tukakuta mlango umefungwa kwa ndani.
Katika kumchungulia tulimwona mtu huyo akiwa amekaa kitandani bila
kujigeuza jambo lililonifanya nipige simu polisi ambao walifika na
kuvunja mlango na kumkuta akiwa amefariki dunia,” alisema mwenyekiti
huyo.
Aliongeza kuwa, katika chumba hicho alichofia mteja huyo, kulikutwa
mabomba mawili ya sindano ambapo moja lilikwishatumika, pia kulikuwa na
mifuko miwili yenye nguo na begi moja.
Polisi waliuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hata
hivyo, ndugu wa marehemu walipatikana na mwili kufanyiwa uchunguzi na
daktari kisha kuuchukua na kuusafirisha kwenda Mwanza kwa mazishi.
0 comments:
Post a Comment