REAL Madrid ya Hispania inatua nchini Agosti 21 ikiwa na nyota wake wa
zamani. Wachezaji kama Luis Figo, Ruud van Nistelrooy, Michael Owen,
Zinedine Zidane watakuwemo kwenye kikosi hicho kilichopewa jina la
Madrid Legend.
Ofisa Habari wa Kampuni ya TSN Limited ambao wanafanikisha ujio wa timu
hiyo kubwa duniani, Dennis Ssebo alisema kuwa wachezaji Cristiano
Ronaldo, Rameres na Iker Casillas watatengeneza matangazo ya ujio wa
timu hiyo nchini.
“Jumamosi tutakuwa Lisbon kutengeneza matangazo ambayo yatarushwa
Hispania na Tanzania kuhusu ujio wa timu hii, wachezaji hao mbali na
kutengeneza matangazo pia tupo kwenye mazungumzo nao ikiwezekana nao
wawe miongoni mwa wachezaji watakaokuja nchini,”alisema Ssebo.
Kikosi hicho kitakapokuwa nchini kitacheza mchezo mmoja wa kirafiki
Agosti 23 na timu ambayo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), itaiunda
ambayo itajulikana kama Tanzania Eleven, mchezo utakaochezwa kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Real Madrid Legend kwenye mkutano huo iliwakilishwa na mkongwe na
kapteni wa timu hiyo, Ruben de la Red aliyeambatana na Rayo Garcia
pamoja na Isaac Recarey Sanchez anayehusika na mambo ya uhusiano ndani
Madrid Legend Club. Walisaini mkataba wa ziara ya timu hiyo nchini na
Mkurugenzi wa TSN Group, Farough Baghoza mbele ya waandishi wa habari
katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Serena jijini Dar es Salaam.
Ssebo alisema timu hiyo itawakilishwa na wachezaji 25 na watakaa nchini kwa siku tatu wakiwa na ratiba mbalimbali.
“Wachezaji hawa wakongwe ambao bado wako fiti na wanacheza wanatazamia kutembelea mbuga za wanyama, “alisema Sanchez.
Aliwashauri vijana wa timu ya Tanzania kujifua kwa kuwa yawezekana
kikosi hicho cha Madrid kiko fiti. Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema;
“Ujio wa timu hii utatupa mafunzo mengi na uzoefu walionao wachezaji
hawa lakini pia watasaidia kuitangaza nchi kwa ujumla.”
0 comments:
Post a Comment