Tuesday, 13 May 2014
Mashabiki 15 Wafa Uwanjani Kinshasa Mechi ya Tp Mazembe Vs AS Vita
Ghasia zilizozuka mwishoni mwa mechi ya soka iliyozikutanisha timu mbili maarufu za AS Vita na TP Mazembe za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zimesababisha watu wanaokadiriwa kufikia 15 kufariki dunia.
Mechi hiyo ambayo ilichezwa Kinshasa nyumbani kwa AS Vita, ilikuwa ya kuamua ni timu ipi itaiwakilisha DRC katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Katika tukio hilo ambalo Watanzania wawili wanaocheza soka ya kulipwa katika timu ya TP Mazembe, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta walikuwapo, watu zaidi ya 20 wameripotiwa kujeruhiwa huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka. Iliwachukua dakika 20, Samatta na Ulimwengu pamoja na wachezaji wenzao wa TP Mazembe kutoka uwanjani baada ya ghasia hizo.
Hali ilivyokuwa
Ghasia hizo zilianza katika dakika tatu za nyongeza wakati winga wa TP Mazembe, Solomon Asante alipokuwa akijiandaa kupiga kona huku TP ya Lubumbashi ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Gladson Awako katika dakika ya 35. Ghafla alirushiwa mawe na mashabiki, ndipo mwamuzi alipoamua kusimamisha mechi baada ya ghasia kuongezeka.
Baada ya kuona ghasia zinazidi kuongezeka, polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi ili kutawanya mashabiki waliokuwa wakipambana na kusababisha watu kukimbia ovyo na kukanyagana na kusababisha baadhi kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Taarifa ya serikali ya DRC inasema kuwa vifo hivyo vimetokana na watu kukanyagana baada ya polisi kufyatua mabomu ya machozi uwanjani na kuwafanya mashabiki kutaharuki. Gavana wa Kinshasa alisema serikali itachunguza kwa kina tukio hilo na waliohusika watachukuliwa hatua kali.
Matukio kama hayo yameripotiwa kutokea DRC kwa nyakati kadhaa hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi. Mwezi uliopita, watu 14 walipoteza maisha katika vurugu zilizozuka wakati wa tamasha la kumkumbuka msanii maarufu wa DRC, King Kester Emeneya
0 comments:
Post a Comment